Tuesday, 25 March 2014

Mzindakaya atema cheche katiba mpya


NA MWANDISHI WETU 
MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Chrisant Mzindakaya, amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutambua kwamba wanatunga katiba ya Watanzania na si watawala.  


Sambamba na hiyo, amepongeza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Ijumaa iliyopita kuwa ilikuwa dira ya majadiliano kwa lengo la kupata katiba bora itakayolinda Muungano.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mzindakaya alisema baadhi ya wanasiasa wametanguliza maslahi binafsi kwa ajili ya kujipatia madaraka badala ya uzalendo na maslahi ya taifa.
“Ni lazima watu watambue kuwa duniani kote watawala ni wa kupita, watakaa madarakani kwa kipindi kifupi na kuondoka, lakini wananchi wataendelea kubaki. Kwa hiyo tuunde katiba kwa maslahi ya taifa na si watawala,” alisema.
Kuhusu hotuba ya Rais Kikwete, Mzindakaya ambaye aliwahi kuwa mbunge kwa miaka 44, alisema ilijaa uzalendo na kuitakia Tanzania amani, umoja, utulivu na usalama. 
Alisema hotuba hiyo ilionyesha dhamira ya dhati aliyo nayo Rais katika kuhakikisha Tanzania inapata katiba mpya itakayokuwa mwongozo kwa taifa kwa miaka 50 ijayo au zaidi.  
“Matakwa ya katiba mpya ni wazo la Rais Kikwete mwenyewe kwani alishasema kuwa wakati umefika wa kuwa na katiba mpya. Ndiyo maana hata hotuba yake ilikuwa na uchambuzi wa kisayansi wa namna katiba mpya inavyopaswa kuwa kiuchumi, kisiasa na kijamii,” alisema.
Hata hivyo, Mzindakaya alisema: “Nimeshangazwa na baadhi ya watu wanaoiponda hotuba ya Rais, watu hao akili zao zimeganda na wanaonekana kutaka mambo yao na si hoja. Duniani kote hotuba ya Rais huwa dira ya kuongoza nchi na katika suala hili la katiba, ndiyo dira ya kuongoza majadiliano kwenye bunge la katiba.” 
Alisema Rais Kikwete ameshamaliza kazi hivyo wanachopaswa kufanya wajumbe wa bunge hilo maalumu ni kuhakikisha wanalinda maslahi ya taifa ikiwa pamoja na kudumisha Muungano. 
Juu ya Muungano, Dk. Mzindakaya alisema serikali tatu ni jambo ambalo haliwezekani kwa sababu hakuna katiba ya Tanganyika, nchi ambayo baadhi ya wanasiasa wanaitaka. 
“Hivi kwa akili za kawaida, unaanza kuengeneza katiba ya Muungano wa serikali tatu wakati serikali mojawapo haipo? Ni jambo ambalo haliwezekani. Kama wana nia ya kufanya hivyo wanapaswa kwanza kuwa na Tanganyika ndipo waendele kwenye Muungano wanaoutaka.
Kama wanataka Tanganyika basi wanapaswa kuahirisha bunge mpaka Tanganyika izaliwe kwanza. Kuendelea na fikra hizo ni sawa kuota ndoto za mchana,” alisisitiza.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru