Tuesday, 18 March 2014

Warioba akumbatia serikali tatu


NA EPSON LUHWAGO, DODOMA
TUME ya Mabadiliko ya Katiba imesema chachu ya uwepo wa serikali tatu ni wananchi kutokuridhishwa na uendeshaji wa muundo wa sasa, ukiukwaji wa Katiba na makubaliano.
Kutokana na hali hiyo, imesema serikali tatu ni jambo lisilokwepeka kama kuna nia ya dhati ya kuimarisha Muungano ambao umedumu kwa miaka 50.


Akiwasilisha Rasimu ya Katiba mbele ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba jana, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, alisema historia na matukio ndani ya miaka 30 iliyopita vimeweka mazingira ya kuwepo dukuduku la watu kutaka serikali tatu.
Jaji Warioba alisema licha ya changamoto kadhaa za kuwepo kwa serikali tatu, ikiwemo gharama za uendeshaji, suala hilo halikwepeki.
Alisema ndiyo maana tangu kuanza mjadala wa katiba suala la muundo wa serikali tatu limechukua nafasi kubwa, kiasi cha kufunika mapendekezo mengine ndani ya rasimu.
Kwa mujibu wa Warioba, wananchi walipotoa maoni kuhusu muundo wa Muungano, waliamini kufanya hivyo kutasaidia kuondoa kero zilizopo.
“Wananchi waliotoa maoni kuhusu muundo wa Muungano kwa Tanzania Bara, asilimia 13 walitaka serikali moja, asilimia 24 serikali mbili na 61 serikali tatu. Kwa Zanzibar, asilimia 34 walipendekeza serikali mbili, asilimia 60 Muungano wa Mkataba na asilimia 0.1 walitaka serikali tatu.
“Taasisi nyingi kama vile vyama vya siasa, asasi za kiraia na jumuia za kidini zilipendekeza serikali tatu. Baadhi ya taasisi za serikali, ama moja kwa moja au kwa tafsiri ya mapendekezo yao, pia zilipendekeza au kukubali muundo wa serikali tatu,” alisema.
Jaji Warioba alisema mapendekezo yenye mwelekeo huo yalitolewa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ambalo lilipendekeza kuwe na mamlaka huru ya Zanzibar, mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya Muungano.
Alinukuu pendekezo la Baraza la Ofisi ya Makamu wa Rais lililosema: “Kuwe na Rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakuu wa serikali washirika wapewe vyeo vingine vinavyoendana na hadhi na mamlaka zao. Pia katika kutaja serikali hizo tatu inabidi zitenganishwe ili serikali ya Muungano ionekane ndiyo ya juu.”
Kutokana na uchambuzi wa hoja hizo, Jaji Warioba alisema inaonyesha dhahiri watu wengi wanapendelea muundo wa serikali tatu.
Alisema utafiti uliofanywa na tume baada ya kupata maoni na hoja mbalimbali ulibaini chanzo cha yote ni kuwepo matatizo yanayoashiria kukiukwa makubaliano ya Muungano, hivyo kuwepo kwa hoja ya kutaka serikali tatu.
Jaji Warioba alitoa mfano wa kile kilichoitwa kuchafuka kwa hali ya hewa kisiasa Zanzibar mwaka 1984, ambacho msingi wake ulikuwa mpango wa baadhi ya viongozi wa Zanzibar kutaka serikali tatu.
Kutokana na hilo, alisema kulitungwa Katiba ya Zanzibar, ambayo iliondoa madaraka ya sheria zinazotungwa na Bunge kutumika moja kwa moja Zanzibar hadi zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi.
“Mwaka 1991 Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza muundo wa serikali tatu. Ingawa pendekezo hili halikukubalika, Zanzibar iliamua kuwa na bendera na nembo yake na baadaye kuweka sharti la kutaka meli zinazoingia kwenye Bandari ya Zanzibar lazima zitumie bendera ya taifa yenye nembo ya Zanzibar.
“Kwa maana nyingine, Zanzibar ikaanza kutumia bendera ya taifa iliyo tofauti,” alisema.
Alisema lingine lililosababisha kuwepo madai ya serikali tatu ni Zanzibar kujiunga na Jumuia ya Nchi za Kiislamu (OIC), ambayo ilisababisha ufa na hata kuibuka kundi la G55 lililoundwa na wabunge kutoka Tanzania Bara, likitaka serikali ya Tanganyika.
Jaji Warioba alisema kuondolewa kwa baadhi ya mambo ya Muungano kulikofanywa na serikali ya Zanzibar ni changamoto nyingine inayoonyesha hakukuwa na nia njema ya kudumisha Muungano.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, sababu nyingine inayowafanya baadhi ya wananchi kutaka mabadiliko ya muundo wa Muungano ni kutokutekelezwa mambo yanayokubaliwa au kuchukua muda mrefu kabla ya kufanyiwa kazi.
“Hata suala la gesi na mafuta ni moja ya changamoto hizo, inakuwaje watu wafike mahali na kusema gesi na mafuta vinavyopatikana Zanzibar ni kwa ajili ya Zanzibar tu na vinavyopatikana Tanzania Bara ni kwa ajili ya Muungano.
“Yapo malalamiko mengi kwa pande zote mbili, ambayo yamesababisha watu kushindwa kuridhika na muundo wa sasa wa Muungano na kutaka mabadiliko. Kwa mantiki hiyo, wengi wanataka muundo mpya wa Muungano ambao ni wa serikali tatu,” alisema.
Alisema hata mambo yaliyofanywa na waasisi na kuwekeana makubaliano si yaliyopo sasa kwa kuwa mengi yamepunguzwa au kukiukwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru