Wednesday, 12 March 2014

Yametimia



  • Sitta achukua fomu kuwania uenyekiti
  • Kanuni za Bunge Maalumu zapita kwa kishindo

Na waandishi wetu, dodoma
SAMUEL Sitta, amechukua fomu kuwania uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, akijinadi endapo atapata nafasi hiyo, atafanya kazi kwa viwango na kasi zaidi ya alivyokuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano.
Uchaguzi huo utafanyika leo, huku Sitta akipewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi. Hadi jana jioni hapakuwa na mjumbe mwingine aliyejitokeza kuchukua fomu.
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akipokea fomu ya kuomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa bunge hilo, alizokabidhiwa na Katibu Muhtasi wa Katibu wa Bunge, Lydia Mwaipyana, mjini,Dodoma,jana. Katikati ni Mjumbe wa Bunge hilo, Dk. Khamis Kigwangwala. (Picha na Yassin Kayombo).

Wajumbe pia wamepitisha kwa kishindo azimio la Kanuni za Bunge, ambazo zitaongoza uendeshaji wa shughuli, hivyo kumaliza vitendo vya aibu vilivyokuwa vimetawala, vikiwemo vya baadhi kutumia lugha za matusi, kejeli na kuzomea.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Sitta alisema iwapo atachaguliwa ataendesha bunge kwa kusimamia kanuni na kutumia busara katika kutoa uamuzi.
“Kwa kutumia uzoefu wangu wa kuwa  Spika wa Bunge la Tisa (2005 hadi 2010), na kwa kuwa umri wangu umeongezeka, ni wazi nitafanya vizuri zaidi katika kuendesha mijadala kwa haki na usawa, bila kutawaliwa na hisia za kisiasa au matakwa ya watu binafsi.
“Najua wako watu wengine ambao si wazoefu wa mambo ya kibunge lakini kutokana na walivyoona mijadala ilivyokuwa ikifanyika wakati wa kujadili kanuni, wamepata uzoefu,” alisema.
Sitta alisema: “Kwa hali hiyo, nitajaribu kuwapa kipaumbele wale ambao walikuwa hawazungumzi mara kwa mara katika vikao ili kusikiliza mawazo na michango yao,” alisema.
Alisema kutokana na kuwepo kamati mbalimbali ana matumaini ataendesha mijadala vizuri kutokana na kupokea mawazo ambayo yatakuwa yamekwisha kufanyiwa kazi.
Kuhusu shinikizo la kiitikadi, alisema hawezi kufanya hivyo kwa sababu kanuni zinazoendesha chombo hicho hazimruhusu kushiriki vikao vya chama kuanzia wakati atakapokalia kiti hicho.
Sitta alichukua fomu akiwa na wapambe Dk. Hamisi Kigwangalah na Paul Makonda.
Katika hatua nyingine, wajumbe jana walipitisha kwa kishindo kanuni za bunge hilo, ambazo zitaongoza uendeshaji wa shughuli bungeni.
Hatua hiyo ilifikiwa kwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge, Pandu Ameir Kificho, kuwahoji wajumbe baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Profesa Costa Mahalu, kuwasilisha maelezo na baadaye kutoa hoja.
Baada ya Profesa Mahalu kuwasilisha maelezo ya awali na kusoma azimio la bunge la kupitisha kanuni hizo, wajumbe kadhaa walisimama na kuchangia, ambao waliliunga mkono.
Profesa Ibrahim Lipumba, aliwaomba wajumbe kuunga mkono azimio hilo kutokana na kazi iliyofanywa na kamati ya Profesa Mahalu kuwa nzuri, na kanuni zinatoa dira ya kule wanakokutarajia.
“Jana (juzi) tuliahirisha Bunge kwa ajili ya kupata muda wa kuzisoma kabla ya kuzipitisha. Lengo letu lilikuwa tuwe na sauti moja, kanuni hizi ni nzuri na zinakidhi mahitaji ya kuendesha Bunge hili la Katiba,” alisema.
Profesa Lipumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema kanuni hizo zimetoa fursa ya wajumbe kuwa huru katika kuchangia bila kushurutishwa au kukandamizwa na chombo chochote.
Dk. Francis Michael, ambaye anawakilisha kundi la wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais, aliunga mkono kwa kusema kanuni hizo zinaonyesha wananchi wana matumaini ya kupatikana katiba mpya.
“Inawezekana kuna mambo yana kasoro ndani ya kanuni hizi lakini ni ukweli usiopingika kwamba, hayawezi kuharibu uzuri wa kanuni hizi. Tutafika mahali tutarekebisha kasoro hizo, hivyo ni vyema tukaunga mkono ili tuendelee na kazi iliyotuleta,” alisema.
Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Jenista Mhagama, aliyesema kanuni hizo zimeandaliwa kwa weledi na umakini mkubwa na wataalamu waliobobea katika sheria.
Alisema kanuni zimezingatia mijadala inayoendelea ndani ya bunge, mustakabali na maslahi ya taifa.
Kwa upande wake, James Mbatia, alisema kuandaliwa kwa kanuni hizo kumewezesha kuandikwa historia mpya ya uhai wa taifa la Tanzania.
“Naunga mkono azimio hili kwa sababu kwa hulka ya binadamu ni kutokukubaliana katika  mambo mengi lakini jambo la msingi na la kujivunia ni kwamba, kanuni hizi zimeandaliwa katika kipindi kifupi.
“Historia inaonyesha kanuni hizi zimeandaliwa kwa wiki tatu, ambao ni muda mfupi ikilinganishwa na nchi zingine ambazo zimeandaa kwa zaidi ya miezi mitano na kuendelea,” alisema.
Hata hivyo, alitaka majadiliano ndani ya bunge yawe na umoja, hekima na mshikamano.
Freeman Mbowe, kwa upande wake, alisema anaunga mkono kwa asilimia 30 na kwamba, jana ilikuwa siku ya 21 tangu kuanza kwa bunge na imeonyesha kipimo cha uvumilivu miongoni mwa wajumbe katika kupitia hatua hiyo.
Alisema katika kipindi chote cha kujadili kanuni kulikuwa na mivutano na majaribu, ambavyo vilitishia kutokufikia muafaka lakini anaamini hatua iliyofikiwa ni nzuri na itakuwa na mwisho mwema.
“Namshukuru Mheshimiwa Joseph Selasini, ambaye alitoa ushauri wa kumtanguliza Mungu kabla ya kuanza shughuli zetu. Hatua hii imefanya miongoni mwetu kulegea hata mapepo yaliyokuwa yametawala hapa kutoweka. Hata wenye mioyo migumu walilegea, hivyo tuendelee kuvumiliana,” alisema.
Wengine waliounga mkono azimio la kupitisha kanuni ni Anna Abdallah, Askofu Amos Muhagachi, Sheikh Mussa Kundecha na Ismail Jussa Ladhu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru