Tuesday, 4 March 2014

CHADEMA waingiza mtambo kutengeza shahada


NA SULEIMAN JONGO, KALENGA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeituhumu CHADEMA kwa kupanga mchezo mchafu ili kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kalenga, mkoani wa Iringa.
Miongoni mwa rafu zinazodaiwa kuchezwa na CHADEMA ni pamoja na kuingiza jimboni humo mtambo maalumu wa kutengeneza shahada bandia watakazozitoa kwa makada wake ili wapige kura.
Tuhuma hizo zilitolewa jana na Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu matukio yanayoendelea wakati huu wa kampeni za uchaguzi huo.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Machi 16, mwaka huu, na CCM itawakilishwa na Godfrey Mgimwa.
Mtenga alisema CCM ina taarifa za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya CHADEMA kuwa, kuna mtambo unaotarajiwa kuingizwa kati ya leo au kesho ili kutengeneza shahada za kupigia kura.
Alisema tayari chama hicho kimeanza kununua shahada za wapiga kura halali wa jimbo hilo kwa lengo la kuzibadilisha picha za ili kuweka za watu waliowandaa ambao si wakazi wa Kalenga.

“Tunazo taarifa za ndani na za uhakika kuwa CHADEMA inataka kuleta mtambo huo ili kutengeneza shahada bandia kutokana na shahada halali walizoanza kununua.
“CHADEMA wamepanga mchezo huo mchafu kwa kushirikiana na baadhi ya walimu ambao hivi sasa wanapewa mafunzo ya namna ya kuutumia mtambo huo ili kufanikisha hujama yao dhidi ya CCM na wana-Kalenga,” alisema.
Kwa mujibu wa Mtenga, walimu 80 wamekutana na CHADEMA na kupewa mafunzo ya namna ambavyo watafanikisha hujuma hiyo siku ya uchaguzi.
Mtenga alisema CCM imekuwa ikifuatilia nyendo za CHADEMA kwa karibu na kwamba kila kitu kinachofanywa na chama hicho hivi sasa Chama kinapata taarifa kwa wakati.
Alisema  licha ya njama hizo, CHADEMA inajisumbua kwa  kuwa CCM ina uhakika wa kushinda uchaguzi huo kwa asilimia kubwa. 
Wakati huo huo, Mtenga alisema baadhi ya vijana wa CHADEMA wamekamatwa na polisi wakiwa na visu, nondo na minyororo ya kunyongea.
Alisema vijana hao walikamatwa jana usiku  ambapo wawili kati yao ni Saitoti Msuva mkazi wa Arusha na Shindo Ndondi.
Katibu huyo alisema vijana hao walikamatwa na polisi jimboni humo na baada ya kupekuliwa walikutwa na silaha hizo ambazo zinadaiwa kuwa na kazi maalumu.
“Aidha, tunayo majina ya vijana wengine wa CHADEMA ambao wametoka nje ya Iringa kwa ajili ya kuleta vurugu siku ya uchaguzi,” alisema.
Hata hivyo, alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi, alisema amepokea malalamiko kutoka vyama mbalimbali vinavyoshiriki uchaguzi huo na kwamba jesdhi hilo limejipanga kusimamia amani na kung’amua vitendo vya uvunjifu wa amani.
Mtenga alikionya chama hicho na kusema CCM imejipanga na kwamba iko macho kulinda kura na wapiga kura hadsi pale Mgimwa atakapotangazwa mshindi.
Uchaguzi huo mdogo unatokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa Kalenga, Dk. William Mgimwa, aliyefariki dunia Januari, mwaka huu, nchini Afrika Kusini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru