NA CHARLES MGANGA, DODOMA
MCHUNGAJI Christopher Mtikila, jana alichafua hali ya hewa baada ya kumvaa Mwenyekiti wa Muda Pandu Ameir Kificho kwamba anamnyima nafasi ya kuzungumza.
Mtikila ambaye ni Mjumbe wa Bunge la Katiba, aliamua kusimama baada ya Kificho kusimama na kusema wachangiaji waliotangulia kuunga mkono azimio la kanuni wanatosha na wamewakilisha mawazo ya wajumbe waliopo.
“Mwenyekiti kwa nini unaninyima haki yangu ya kuzungumza? Kuzungumza ni haki yangu ya msingi. Hivi ni sababu gani hunipi nafasi ya kuongea.
“Siwezi kukuheshimu wakati wewe hulindi heshima yangu. Mwenyekiti ni haki yangu kuzungumza, ninayo ya kuzungumza, nipe nafasi. Umekuwa ukiwapa nafasi watu ambao umewapanga wewe. Umekuwa ukifanya hivyo mara zote,” alilalamika.
Wakati akiendelea na malalamiko hayo, ilisikika tena sauti ya mjumbe mwingine, Felix Mkosamali, ambaye naye aliungana na Mtikila kwa kusema, Kificho amekuwa akipendelea watu wa kuzungumza ndani ya Bunge hilo.
Mkosamali ambaye ni Mbunge wa Muhambwe (NCCR Mageuzi), alisema hawezi kuvumilia hali hiyo ambayo haina usawa ndani ya Bunge kwa mwenyekiti kuwapa nafasi watu anaowataka.
“Mara zote wengine tumekuwa tukinyimwa nafasi ya kuzungumza. Hatuna sababu ya kuunga mkono kazi mbovu ya kuandaa kanuni iliyofanywa na Kamati ya Kanuni.
“Kwa nini Mwenyekiti hutupi nafasi ya kuzungumza sisi ambao tunapinga utengenezaji wa kanuni hizo mbovu,” alisema.
Akizungumza nje ya ukumbi wa bunge, Mtikila alisema azimio hilo la kanuni lilipitishwa kwa hila kwa ajili ya kulinda maslahi ya wakubwa.
“Ukweli ni kwamba hili azimio limepitishwa kwa hila, kwanza tulivutana sana ndani ya UKAWA (Umoja wa Kambi ya Wapinzani), sasa hayo ndiyo yaliyotokea,” alilalamika Mtikila.
Mtikila alisema viongozi wa UKAWA ambao walikutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ndiyo walibadili upepo huo.
Alisema, ilifikia hatua umoja wao haukubaliki kwa ajili ya kulinda maslahi ya wakubwa.
“Hii ndiyo rushwa na ufisadi uliofanyika katika hatua hii ya kupitisha azimio la katiba. Kwa kweli limepita kwa hila,” alisema Mtikila.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru