Na Suleiman Jongo
MGOMBEA ubunge katika uchaguzi mdogo Kalenga
kwa tiketi ya CCM, Godfrey Mgimwa, amesema ameamua kuwania kiti hicho ili
kuwatumikia wananchi na si kusaka utajiri.
Akiwahutubia wananchi wa kata ya Nzihi jana,
Mgimwa alisema kabla ya kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho alikuwa akifanya
kazi kwenye moja ya benki hapa nchini na kumpatia fedha za kutosha.
Mgimwa alisema lengo na ndoto zake ni kuona
jimbo la Kalenga, ambako ndiko iliko asili yake, linapata maendeleo kwenye sekta
mbalimbali.
Alisema moja ya vipaumbele vyake ni pamoja na
kuharakisha mtandao wa mawasiliano hususan kwenye maeneo ambayo bado hayana
huduma hiyo kwa kiwango cha kutosha.
"Najua moja ya changamoto kubwa katika jimbo letu ni kusuasua kwa mawasiliano kutokana na uchache wa minara, naahidi kulishughulikia hilo mapema iwezekanavyo iwapo nitapata ridhaa ya kuwa mbunge wa Kalenga," alisema.
Alisema kiu yake ni kuona Kalenga inapiga
hatua kimaendeleo na kwamba ndiyo iliyomrudisha nchini kutoka nje alikokuwa
akisoma na kuwa na uwezo mkubwa wa kuendesha maisha huko endapo angetaka iwe
hivyo.
"Niliona ni vyema elimu niliyoipata nje ikawanufaisha Watanzania wenzangu ambao walichangia kwa kiasi kikubwa kufika hapa nilipo sasa," alisema.
Alifafanua mafanikio ndani ya Kalenga,
yatafikiwa iwapo kutakuwa na ushirikiano kati ya viongozi na wananchi.
Mgombea huyo alisema anajiamini kuwa ataweza
kuzikabili changamoto zitakazojitokeza kwa kushirikiana na wananchi.
Aidha, aliwataka wakazi wa Nzihi kutokakubali
kudanganywa na wapinzani kuwa serikali iliyoko madarakani haijafanya chochote
cha maendeleo.
Mgimwa aliwaomba wapiga kura hao Machi 16
mwaka huu, kuipa kura CCM ili iwaletee maendeleo.
Jimbo hilo lina kata 13 na zaidi ya vijiji 40
ambapo kwa mujibu wa daftari la kdumu la wapiga kura kuna wapigakura 85,051
walojiandokisha.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru