Na Epson Luhwago, Dodoma
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, ambaye pia ni mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), amechaguliwa kwa kishindo kuwa mwenyekiti wa bunge hilo.
Sitta katika uchaguzi uliofanyika jana, alishinda kwa kura 487 kati ya 563 zilizopigwa sawa na asilimia 86.5. Mpinzani wake Hashim Rungwe, alipata kura 69 sawa na asilimia 12.3, huku kura saba ziliharibika.
Wajumbe wengine waliochukua fomu ni Dk. Terezya Huvisa na John Chipaka, ambao hawakuzirejesha.
Sitta alimshukuru Mungu kwa kumwezesha kuchaguliwa na CCM kwa kumpitisha. Pia alimpongeza Andrew Chenge, kwa kujitoa ndani ya Chama.
Dalili za ushindi wa Sitta zilionekana tangu alipotangazwa kupitishwa na wajumbe kutoka CCM kuwa mgombea wa nafasi hiyo. Muda mfupi kabla ya kikao cha bunge kuanza saa 10 jioni, vipeperushi vilisambazwa kumnadi.
Ndani ya ukumbi wa bunge wajumbe walikuwa na vipeperushi hivyo, ambapo Sitta alisimama kwenye lango kuu la kuingilia ukumbini na kuwasalimu wajumbe akisema: “Jamani mnaniona, mimi mzima wa afya.”
Alipoingia ndani ukumbi ulilipuka kwa vifijo na nderemo na hata Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo alipotangaza jina lake kulikuwa na shamrashamra.
Alipopewa nafasi ya kujieleza, Sitta alisema hana maelezo marefu kwa kuwa mambo yake yote ameyaweka kwenye vipeperushi na kwamba, yeye siku zote ni mtu wa kujipanga.
Katika kipeperushi aliweka dira inayosema: “Bunge la Katiba lenye mjadala wa kushindanisha hoja kwa hoja kwa maslahi ya taifa, ili kuwaletea Watanzania ndani ya muda Katiba maridhawa inayokidhi matarajio ya wengi na inayojenga matumaini yao ya utawala bora na maendeleo endelevu kwa wote.”
Alijinadi kuwa mpenda demokrasia, mtetezi wa haki na maslahi ya anaowaongoza, mzalendo asiyetumia vibaya madaraka aliyokabidhiwa, mtetezi wa maendeleo ya wanawake, wanyonge, walemavu na asiyependa ubaguzi wa aina yoyote.
Sitta alisema ni mtu wa viwango na kasi na ataendesha bunge kwa staili hiyo, kutokana na uzoefu alioupata alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ndugu zangu wengi mnanijua kutokana na uzoefu wangu. Kuniweka kwenye kiti hiki ni sawa na kumrejesha chura kwenye dimbwi la maji, kwa vyovyote vile ataogelea tu,” alisema.
Alipoulizwa na David Silinde kama atawafikisha Watanzania katika kupata katiba bora na kuepusha hatari ya bunge kuvunjika kabla ya kumalizika mchakato, alisema hilo halitawezekana.
Sitta alisema jambo la kwanza ni kumuomba Mungu awaepushe na hilo na atahakikisha anapambana na wale wote wenye nia ya kufanya mchakato huo uwe na mushkeli.
“Wapo watu wawili watatu ambao siku zote ni wapinga Muungano na wanataka uvunjike. Watu hao nitapambana nao na wengi mnajua msimamo wangu kuhusu Muungano,” alisema.
Alisema wananchi wana imani na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kwamba, ni watu wenye uwezo wa hali ya juu ndiyo maana Rais Jakaya Kikwete, amewateua na ni viongozi katika jamii walizomo.
Sitta aliamsha kofi, nderemo na vifijo baada ya kumaliza kujieleza na kuomba kura, pale alipokwenda kupeana mkono na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Pia walikumbatiana baada ya Sitta kutangazwa mshindi.
Lowassa na Sitta wamekuwa wakielezwa ni mahasimu wa kisiasa, hususan tangu Lowassa alipojiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2008, kutokana na sakata la mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura wa Kampuni ya Richmond Development Corporation LLC.
Rungwe aliwaacha hoi wajumbe alipojinadi yeye ni Mtanzania wa kwanza mweusi kuanzisha duka la kuuza magari.
Alisema angeweza kuongoza bunge vizuri kwa kuwa ni mwanasheria na wakili wa kujitegemea anayeshinda kesi kila siku mahakamani. Rungwe, aligombea urais mwaka 2010, jambo alilosema lingemwezesha pia kuongoza bunge.
Thursday, 13 March 2014
Sitta atikisa Bunge
01:30
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru