Na Suleiman Jongo
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema
kinasikitishwa na baadhi ya vyama vya siasa ambavyo vimejenga utamaduni wa
kuwatumia vijana kufanya vurugu na
maandamano yasiyo na tija zaidi ya kuweka mazingira ya umwagaji damu.
Hayo yalisema jana na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Iringa Joyce Nsambatavangu,
wakati akimdani mgombea wa CCM katika jimbo la Kalenga mkoani hapa, Godfrey
Mgimwa.
Alisema ni jambo la ajabu wakati serikali
inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuandaa vijana, lakini wanapofikia umri wa
miaka 15 na kuendelea, vinatokea vyama vya siasa vinatumia nafasi ya uwepo wao
kufanya vurugu.
"Ni jambo baya kuona vijana ambao wamegharamiwa kwa fedha nyingi wanatumika kuvuruga amani ya nchi hii na katika hilo Chama na serikali havitakubali yafanyike," alisema.
Alisema ni vyema Watanzania watambue baadhi
ya vyama vya upinzani kuwa havina nia njema na taifa kwa kuwa viko tayari
kufanya kila aina ya hila kuhakikisha amani ya nchi inatoweka na wanaotumika
kufanya hilo ni baadhi ya vijana ambao wanatumiwa kwa maslahi ya vyama hivyo.
Alisisitiza kuwa CCM haiko tayari kuona vijana ambao wamekuzwa kwa
gharama kubwa wanaingizwa kwenye makundi ya vurugu na fujo na muda mwingi
ukitumika katika maandamano yasiyo na tija.
"Inasikitisha baadhi ya wanasiasa ambapo wanatumia kila mbinu kuhamasisha vijana kufanya vurugu na matukio mengine yanayoashiria umwagaji damu nchini,"alisisitiza
Pia alisema wananchi washirikiane na CCM
katika kuleta maendeleo kwa kutumia makundi yote nchini na huku akitumia nafasi
hiyo kuwataka wachukie vyama vinavyohamasisha vurugu na fujo kwa kutumia
vijana.
Pamoja na hayo, aliwataka
wananchi kutofanya makosa katika siku ya uchaguzi ambayo ni Machi 16, mwaka
huu, kwa kumpa kura Mgimwa ili aweze kuleta maendeleo katika jimbo hilo na
kwamba hakuna sababu ya kuchagua upinzani.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru