Tuesday, 25 March 2014

Kinana: Ridhiwani hatafuti umaarufu


Na Mwandishi Wetu, Chalinze
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema mgombea wa ubunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, hagombei kwa kutaka umaarufu bungeni au kwenye jamii bali ni kushirikiana na wakazi katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Kinana

Pia kimeahidi kushirikiana naye bega kwa bega atakapochaguliwa kushika nyadhifa hiyo katika kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa Chalinze.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema hayo jana wakati akimnadi Ridhiwani katika kata za Mdaula, Ubena na Msolwa. Alisisitiza kuwa CCM iko tayari kushirikiana naye kwa sababu inaamini suluhisho la matatizo ya wakazi wa jimbo hilo ni kumchagua Ridhiwani.
“Ridhiwani si mgeni wa siasa, alianzia tangu utotoni hivyo hagombei kwa ajili ya kutafuta umaarufu wala kutaka utukufu. Mna kila sababu ya kuwa kifua mbele kwani ni mtu anayejua kero zote za jimbo na atakayetetea maslahi ya wananchi ikiwemo kusaidia matatizo yote yanayowakabili,” alisema.
Kinana alisema kwa sasa siasa za kukebehiana zimepitwa na wakati hivyo Ridhiwani ana uhakika kutokana na kujiuza kwa sera za Chama chake ambazo si za kubabaisha.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Ridhiwani alisema changamoto nyingi zinajirudia katika maeneo mengi ikiwemo migogoro ya ardhi, afya, elimu,  maji na vijana kuhitaji mitaji ili kujikwamua kiuchumi.
Alibainisha kuwa katika vipaumbele vyake endapo atachaguliwa atahakikisha anashughulikia makandarasi wa miradi ya maji na barabara ambayo mingi inakwamishwa au kutomalizika kwa wakati kwa ajili yao. Alisema makandarasi wasiotekeleza majukumu yao lazima wawajibishwe.
Pia aliahidi kuongeza zahanati katika kila kijiji ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Kwa  upande wa elimu, alisema atahakikisha anashirikiana na halmashauri kuongeza vyumba vya madarasa, maabara, kujenga matundu ya vyoo na katika shule za sekondari kuziwekea umeme ili  kuwawezesha wanafunzi kujisomea nyakati za usiku.
Kuhusu  kuwezesha vijana kujikwamua kuchumi, aliahidi kuzungumza na idara husika itakayoweza kuongeza mfuko wa fedha za mikopo kwa vijana na wanawake ili waweze kujiinua kimaisha.
Katika kilimo, alisema atajitahidi kuwasaidia wakazi hao kuondokana na kilimo cha jembe la mkono na kuwawezesha kutumia matrekta ambacho kitawaongezea tija.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawamba, ambaye ni mbunge Bagamoyo, aliwaomba wakazi wa jimbo hilo kumchagua Ridhiwani kwa sababu ana uwezo wa kupigania matatizo yanayowakabili.
Awali, msafara huo ulifungua mashina mawili ya UVCCM Ubena Zomozi likiwemo la madereva boda boda na la wajasiriamali wauza koroshon

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru