Wednesday, 5 March 2014

Mangula: CHADEMA haina ubavu kwa CCM


NA SULEIMAN JONGO, KALENGA

PHILLIP Mangula, amesema ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni makini na kinaendesha mambo yake kwa mpangilio, hivyo, CHADEMA haina ubavu wa kushindana nacho.


Pia, amekifananisha na wachuuzi wa biashara za mkononi kwa kuwa hakina maeneo rasmi ikiwemo ofisi kwa ajili ya kufanyia shughuli zake wala mfumo wa uongozi unaoeleweka.
Alisema CCM imekwenda Kalenga kuwaeleza wananchi utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo kupitia sera zake, huku CHADEMA kikienda kwa ajili ya kuwadanganya na kuwafanyia vurugu.
Mangula ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, ndio msimamzi wa kampeni za Chama hicho katika jimbo la Kalenga mkoani Iringa.
Aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wa Kata ya Mugama.
Alitoa kauli hiyo baada ya kupewa taarifa ya maandalizi ya uchaguzi na Katibu wa CCM Kata ya Mugama, Sylvester Samon, kuwa CHADEMA hakina dalili za kushindana na CCM wala kushinda.
Alisema CHADEMA haina ofisi hata moja katika kata nzima ya Mugama, jambo linalo ilazimu kutumia mbinu chafu ikiwemo ya kushusha bendera za CCM na kuchana mabango ya mgombea wake, Godfrey Mgimwa.
Baada ya kupewa taarifa hiyo, Mangula alisema CHADEMA haina ubavu wa kupambana na CCM na kwamba, kimekosa mwelekeo Kalenga.
“CHADEMA hakina hata ofisi moja katika kata nzima, hivi unaweza kusema kina dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo au wanataka kudanganya wananchi kama kawaida yao,” alisema Mangula.
Alisema CCM imejipanga kupata ushindi wa kishindo na mafanikio katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 inadhihirisha hilo bila kuacha shaka.
Mwenyekiti wa CCM kata ya Mugama, Betha Luhavi, alisema wana taarifa kamili kuhusu wapiga kura wa eneo hilo hivyo, watahakikisha hakuna mvamizi.
Alisema viongozi na wapenzi wa CCM watakuwa mstari wa mbele kuhamasisha amani kipindi chote cha kampeni na siku ya uchaguzi, ili kuhakikisha unafanyika kwa amani.
Aidha, alisema CCM itashirikiana na vyombo vya dola kufichua uhalifu wa aina yoyote unaolenga kuvuruga uchaguzi na amani.

Wafuasi waikimbia CHADEMA

Wakati kukiwa na dalili zote za kuambulia patupu, CHADEMA imeendelea kupatwa na majanga baada ya wanachama na viongozi wake kukihama.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Lupembelwasemga katika jimbo la Kalenga, Ezekiel Kibiki, ametangaza kukihama na kujiunga na CCM.
Kibiki alisema ameamua kurejea CCM kutokana na kukerwa na siasa za uzushi na vurugu zinazohamasishwa kwa wananchi.
Akizungumza mbele ya viongozi wa CCM, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Lupembelwasenga, Kibiki alisema amerudi nyumbani ambapo kuna kila kitu ikiwemo maendeleo ya kweli.
Alisema CCM imefanya mambo mengi na kazi kubwa, hivyo haoni sababu ya kuendelea kukaa upinzani bila sababu za msingi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe, alisema ni vyema wananchi wakamchagua Mgimwa kwani anafahamu vyema kero zinazowakabili.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru