NA MWANDISHI WETU, KIBAHA
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amewaagiza viongozi wa Chama kuwahoji watendaji wa serikali ambao utendaji wao umekuwa wa kusuasua.
Abdulrahman Kinana |
Alisema ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ya haraka waliyotarajia ni lazima viongozi wa CCM wakaendelea na utaratibu wa kuwahoji watendaji wa serikali bila kuwaonea haya haya.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi, Kibaha Vijini, Kinana alisema Watanzania hawataki kudanganywa, hivyo ni lazima kile walichoahidiwa watekelezewe kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
“Tujenge tabia ya kuwa wa kweli kwa wananchi katika kuwatumikia na wale watakaoshindwa ni fursa nzuri wakaacha kazi wenyewe,” alisema na kuongeza: ‘’Ahadi ni deni hivyo ni lazima zitekelezwe kwa kuwa wananchi hawataki maneno, wanahitaji huduma.”Alisema wananchi wanatakiwa kuhudumiwa kwa kuwa ndio waajiri wa serikali na watendaji wake na kuwataka kuwa wakali na kuchukua hatua pale mambo yanapokwenda kinyume.
Awali, akizungumza na viongozi wa CCM katika ofisi za CCM za Wilaya ya Kibaha Vijijini, Kinana aliwaagiza viongozi hao katika ngazi zote kuwahoji bila kuwaonea aibu wafanyakazi wa serikali ambao utendaji wao ni wa kusuasua.
“Najua jambo hili litaleta ugomvi na migogoro, lakini bila kuogopa, lazima tuwaulize pale tunapoona mambo hayaendi sawa. Mbona wakati wa uchaguzi hatuwaoni, sisi ndio tunaoimba katika mikutano ya kampeni kutatufa ushindi,” alisema.Kinana alisema CCM inapaswa kusimamia na kufuatilia utendaji wa serikali ili kujiridhisha kuhusu hali ya utekelezaji wa ahadi ilizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi kupitia Ilani zake.
Kinana alisema kutokana na kuwa katika uchaguzi ujao Wana-CCM ndio watakaoulizwa na wananchi kuhusu utekelezaji wa ahadi walizotoa katika kampeni zilizopita, tutashikana mashati na ikishindikana, tutakabana koo, lengo likiwa kupata majibu mazuri ya kuwapelekea wananchi.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kibaha Vijijini, Aboud Abuu Jumaa, ametoa pikipiki tisa na baiskeli 87 kusaidia utekelezaji wa shughuli za Chama jimboni humo.
Vyombo hivyo vya usafiri vyenye thamani ya sh. milioni 40, ambavyo Kinana alivikabidhi katika mkutano huo wa hadhara, vitagawiwa kwa kata na matawi ili vitumike katika kufanikisha shughuli za Chama.
Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Jumaa alisema umepata mafanikio makubwa katika sekta za makazi, ambapo jumla ya viwanja vipya 3,228 vimepimwa, huku vijiji mbalimbali, vikiwemo, Misufini na Kwala vikifikishiwa huduma ya umeme.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru