Wednesday, 12 March 2014

Wanaomiliki vitalu kuchunguzwa, kushitakiwa


Na Hamis Shimye
SERIKALI imesema inawafutilia wamiliki wa vitalu na wakibainika wanashiriki uwindaji haramu, watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Imesema imekuwa ikipambana kwa kiasi kikubwa na ujangili nchini, ingawa kuna baadhi ya watu hawataki kuthamini mchango wake.


Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, walisema hayo jana, Ikulu, mjini Dar es Salaam, Rais alipopokea msaada wa magari 11 aina ya Land Rover.
Magari hayo yametolewa msaada na Taasisi ya Frankfurt Zoological kutoka Ujerumani, kwa ajili ya kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya  ujangili nchini.
Rais Kikwete alisema serikali imefanya kazi kubwa katika kupambana na ujangili na bado inaendelea, kwa kuwa sekta ya utalii ina umuhimu mkubwa.
“Wapo wasioamini jitihada zetu, lakini msaada huu umedhihirisha ni namna gani tunavyopambana, hususan kutokana na utalii kuchangia pato kubwa la uchumi,’’ alisema.
Rais Kikwete alisema ana matumaini magari hayo yatatumika vyema na hata kuendeleza harakati za serikali katika kupambana na ujangili.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, magari matano kati ya hayo itapatiwa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa ajili ya hifadhi ya Serengeti na sita yatapelekwa kwa Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Nyalandu kwa upande wake alisema msaada huo unaonyesha ni jinsi gani baadhi ya nchi zipo pamoja na Tanzania katika mapambano ya ujangili, ingawa wapo wachache wanaowabeza.
Alisema nchi imejipanga kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Operesheni Tokomeza Ujangili muda wowote kuanzia sasa.
“Tutaanza operesheni muda wowote kuanzia sasa lakini nawaomba wafugaji waondoe mifugo iliyoingia katika hifadhi, na waache kuchunga sehemu hizo, kwa kuwa operesheni ikianza serikali haitaki lawama kutoka kwa wafugaji,’’ alisema.
Alisema serikali imepata taarifa ya kuwepo baadhi ya wamiliki wa vitalu wanaoendesha biashara ya uwindaji haramu na uchunguzi umeanza.
Nyalandu alisema atakayebainika atachukuliwa hatua.
Waziri aliwataka wananchi kuachana na ujangili, na hata kuziambia familia zao zisifanye ujangili kwa kuwa Operesheni Tokomeza Ujangili ya sasa haitamuacha mtu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Frankfurt Zooligical, Robert Muir, alisema msaada huo unatokana na ushirikiano uliopo kati ya taasisi hiyo na serikali.
Alisema ushirikiano huo ulisaidia kufanyika sensa ya wanyama katika ikolojia ya Selous, na magari hayo yatasaidia jitihada za serikali katika kupambana na ujangili.
Balozi mdogo wa Ujerumani nchini, Hans Koeppel, alisema ana matumaini msaada huo utaongeza kasi ya kudhibiti ujangili.
Naye Mwakilishi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Fillberto Sebrogondi, alisema msaada huo umetolewa wakati muafaka na utasaidia kuongeza nguvu za serikali katika mapambano hayo.
Msaada huo ni wa awamu ya pili, ambapo magari tisa aina ya Toyota Land Cruiser yalitolewa kwa Idara ya Wanyamapori na kusambaza bunduki 500 aina ya AK 47 kwa askari wa wanyamapori katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru