Wednesday 19 March 2014

Kificho amkana Warioba


NA EPSON LUHWAGO
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, amemkana Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na baraza.
Kificho, ambaye ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema hayo jana, siku moja baada ya Jaji Warioba kuwasilisha bungeni Rasimu ya Katiba.


Jaji Warioba alisema mapendekezo yenye mwelekeo wa kuwepo serikali tatu yalitolewa pia na Baraza la Wawakilishi, lililopendekeza kuwe na mamlaka huru ya Zanzibar, mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya Muungano.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 jana, Kificho alisema waraka uliotolewa na Baraza la Wawakilishi haukupendekeza hivyo, bali hiyo ni tafsiri ya Jaji Warioba na tume.
“Tulichosema katika waraka ule juu ya muundo wa Muungano ni kwamba, kutokana na Baraza kuwa la mchanganyiko, wajumbe kutokana na vyama vyao (CCM na CUF) hatutoi pendekezo lolote kwa kuwa kila upande una maoni yake,” alisema.
Alisema ndani ya Baraza la Wawakilishi, CCM inataka muundo wa sasa wa serikali mbili, wakati CUF haina msimamo kamili kwa kuwa kuna wakati inataka serikali tatu na mwingine serikali mbili.
Kificho alisema katika waraka wa baraza uliowasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hakuna sehemu inayoeleza kuwe na serikali tatu bali hiyo ni tafsiri ya tume.
Alisema alikuwa mjumbe wa Tume ya Nyalali ya mwaka 1991 iliyokuwa na wajumbe 22 na katika suala la serikali tatu, wajumbe tisa, akiwemo yeye na Profesa Haroub Othman (sasa marehemu) walipinga.
Kwa mtazamo wake, Kificho aliyekuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, serikali tatu hazikubaliki kwa kuwa uwepo wake ni kuvunja Muungano.
“Serikali tatu ni kuvunja Muungano, ikiwa hivyo, tutakuwa na serikali mbili zenye nguvu na ile ya Muungano itakuwa dhaifu inayoelea elea tu,” alisema.
Alisema katika miaka 50 ya Muungano kuna mambo mengi yamefanyika, ikiwemo Watanzania kuwa wamoja na wanaoishi kwa amani na mshikamano.
Hata hivyo, alisema kuna kero kadhaa ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi ili kudumisha Muungano na kwamba,
yaliyotajwa kwenye rasimu kuwa changamoto au upungufu, yanazungumzika na kupatiwa ufumbuzi, lengo likiwa kuufanya Muungano kuwa imara.
KINGUNGE AMSHANGAA
Mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale -Mwiru, ameijia juu tume kwamba imefanya kazi ambayo haikutumwa ya kupendekeza serikali tatu.
Kingunge ambaye ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema jana kuwa, tume imekiuka hadidu za rejea, ambazo mojawapo inataka kulinda na kudumisha Muungano, kwa kuwa mapendekezo yake ni ya kuuvunja.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa na TBC1 jana, alisema ameshangazwa na tume chini ya Jaji Warioba, kwa kukiuka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
“Warioba na wenzake walipewa kazi ya kuwauliza wananchi watoe maoni  juu ya katiba mpya kwa lengo la kulinda na kudumisha Muungano. Wameacha waliyotumwa na kutuletea wanayoyataka. Hata katika uwasilishaji rasimu amejikita zaidi katika yale wanayoyataka na ya wananchi wameyaweka pembeni.
“Tume iliambiwa izingatie uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haikuheshimu hayo na matokeo yake imependekeza shirikisho lenye washirika wawili, ambao ni Zanzibar na Tanganyika,” alisema na kuongeza:
“Hawazungumzii Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, badala yake Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo zilifutika kwa kuungana ili kuwa na moja kubwa zaidi. Wanafufua jamhuri mbili, wanapata wapi mamlaka hayo?”
Alisema haiwezekani kuwa na nchi tatu ndani ya taifa moja. “Kwa vyovyote vile, huwezi kuwa na mtu mwenye uraia wa nchi mbili katika nchi tatu.
“Ilichokifanya tume, badala ya kujenga imebomoa. Kama ni kero hata kaya ina kero zake, huwezi kusema kwa kuwa mimi na mke wangu tuna ugomvi basi tuachane, hiyo si sahihi.
“Matatizo yanaletwa na wanadamu na watu wa kuyatatua ni wanadamu wenyewe. Vivyo hivyo, hata kwa suala la Muungano kero zilizopo zimesababishwa na watu, hivyo ni watu wenyewe ndio wa kuzitatua,” alisema.
Alisema kwa kupendekeza muundo wa serikali tatu, tume ya Warioba imeshindwa kutafakari matokeo na athari zinazoweza kujitokeza.
Kingunge alisema ilichopaswa kufanya tume ni kuziainisha kero zilizopo na kutoa njia ya kuzitatua ndani ya Muungano uliopo na si kuleta pendekezo la kuwafarakanisha wahusika.
Alisema wamesikia yaliyomo ndani ya  Rasimu ya Katiba, hivyo kazi ni kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutafakari kwa kina na kuandika katiba.
Kingunge aliasa wajumbe kulinda na kudumisha Muungano na kutambua wao ni nani, wametoka wapi, wako wapi na wanataka kwenda wapi.
“Tukishajitambua na tukaelewa kwa kina historia ya Muungano, tusiingie mahali tukafanya uamuzi ambao utatufanya tujute siku zijazo.
“Kitendo cha Tanganyika na Zanzibar kuungana mwaka 1964 kilikuwa cha kihistoria na cha kimapinduzi. Lengo lilikuwa tuwe na taifa moja kubwa na lenye nguvu. Miaka 50 imepita tunataka kuuvunja, tunakwenda wapi?” alihoji.
Alisema baada ya miaka 50 ya Muungano, uamuzi wa kuwa na katiba mpya ni muafaka lakini inayotakiwa ni yenye kulinda Muungano na si kuuvunja.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru