Tuesday, 18 March 2014

TCRA yabaini udhaifu wa vyombo vya habari


NA RACHEL KYALA
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imebaini kuwepo kwa utendaji na maslahi duni katika vyombo vya habari.
Pia, imebaini mazingira duni ya kufanyia kazi katika vyombo vingi vya habari hususan redio na luninga kwa upande wa vitendea kazi na wanataaluma wasio na ufanisi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Injinia Margaret Munyagi, alisema waliyabaini hayo baada ya kufanya ziara kwenye baadhi ya vyombo hivyo, ambapo walishauri wamiliki kufanya maboresho ili kuleta ufanisi.
“Wajibu wa kamati ni kufuatilia, hivyo tunavitaka vituo vya utangazaji hususan redio na luninga kuzingatia kanuni za maudhui ya utangazaji ili kutimiza jukumu lake la kuendeleza uzalendo, uchumi na maendeleo ya nchi kwa jumla,” alisema.
Alisema vituo vyote vya utangazaji vihakikishe vinarusha matangazo salama yasiyo na uchochezi kwani vikitumika vibaya vinaweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi.
Injinia Margaret, alisema Kamati ilikutana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na kumshauri kuhusu kuwepo kwa Bodi ya Utangazaji.
Pia kuundwe sera mbalimbali kama ilivyo kwa taaluma nyingine nchini na walikubaliana kuanza kwa mchakato huo hivi karibuni.
Alisema kamati hiyo imepanga kutembelea vituo vya utangazaji vya Kanda ya Mashariki.
Kamtihiyo jana ilitarajia kianza ziara hiyo mkoani Dar es Salaam, ambapo walitarajia kutembelea Taasisi ya Utangazaji Tanzania (TBC).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru