Tuesday, 4 March 2014

Kulangwa Mhariri Mtendaji mpya UPL

NA MWANDISHI WETU
 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemteua Joseph Kulangwa, kuwa Mhariri Mtendaji mpya wa kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL), inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.

MHARIRI Mtendaji mpya wa Kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL), Joseph Kulangwa,akitembelea ofisi za kampuni hiyo, Lumumba, Dar es Salaam, alipoanza kazi jana. Kushoto ni Meneja Biashara wa UPL, Esther Paul na katikati ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa UPL, Suleiman Waziri. Kulangwa anachukua nafasi ya Josiah Mufungo ambaye amestaafu kazi. (Na Mpigapicha Wetu).
Kulangwa (pichani) ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mhariri wa Habari Leo, gazeti dada la Daily News linalochapishwa na kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) Limited, anachukua nafasi ya Josiah Mufungo, ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria.
Mhariri Mtendaji huyo mpya aliripoti jana na kupokewa na uongozi na baadhi ya wafanyakazi. Alianza kazi rasmi jana hiyo hiyo.
Hata hivyo, Kulangwa si mgeni ndani ya UPL kwani aliwahi kufanya kazi katika kampuni hii, wakati huo ikiitwa Shirika la Magzeti ya Chama (SMC) katika nafasi mbalimbali ikiwemo ya Mhariri wa Makala wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo.
Aliondoka SMC mwaka 1997 na kujiunga na Business Times Limited (BTL) ambako alifanya kazi na kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya Mhariri Mkuu wa Majira. Aliondoka BTL katikati ya miaka ya 2000 na kujiunga na TSN ambako alikuwa mmoja wa wahariri waanzilishi wa Habari Leo.
Kulangwa ni msomi mwenye shahada ya kwanza ya sayansi jamii katika elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia ana stashahada ya elimu kutoka Chuo cha Ualimu Dar es Salaam (Chang’ombe) ambacho sasa ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE).
Licha ya elimu na taaluma hizo, Kulangwa amepitia mafunzo mbalimbali ya muda mfupi katika masuala ya uandishi wa habari ndani na nje ya nchi. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru