NA SELINA WILSON
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakishindani na wapinzani bali na matatizo ya wananchi.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema hayo jana, alipozindua kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Chalinze, kwenye viwanja vya Polisi.
Uzinduzi wa kampeni za CCM ulipambwa na burudani zikiongozwa na kundi la TOT, ngoma za asili na Mwinjuma Muumini. Kinana na ujumbe aliofuatana nao aliingia uwanjani akiongozwa na msafara wa vijana waliokuwa wamepanda pikipiki.
“Tunatambua hapa hatushindani na upinzani, bali tunashindana na matatizo ya wananchi, kwa Chalinze atakayesimamia hilo ni Ridhiwani Kikwete,” alisema.
Alisema CCM ni Chama chenye kuleta majawabu kwa Watanzania, hivyo wananchi wasikubali kurubuniwa na wapinzani.
Kinana alisema kuna wapinzani ambao ni watu wa ovyo, wanaotembea na mitambo ya kutengeneza chuki, ugomvi na uongo miongoni mwa Watanzania.
Alisema baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikitembeza bakuli kuwataka wananchi kuvichangia, badala ya kuwaletea maendeleo.
Katibu Mkuu aliyemnadi Ridhiwani kwa wananchi, alisema ni mgombea kijana atakayeweza kukaa na vijana kutatua kero zao kwa karibu kuliko mtu mwingine.
Kutokana na hilo, aliwaomba wananchi wamchague kwa kura nyingi za kishindo.
Aliwaomba vijana kuwa karibu na Ridhiwani kwa kuwa CCM inajipanga kuhakikisha kazi zote za ukandarasi wanapatiwa, hivyo kwa utaratibu utakaopangwa, yeye ndiye atakuwa kiunganishi.
“Chagueni mbunge atakayetatua matatizo ya wananchi, atakayekwenda kuungana na asilimia 74 ya wabunge wa CCM kufanya kazi za wananchi,” alisema.
Kinana alisema CCM inatambua matatizo ya Chalinze, yakiwemo ya maji, ambayo Ridhiwani atakuwa na nafasi ya kuendeleza yaliyoachwa na aliyekuwa mbunge Said Bwanamdogo, aliyefariki dunia hivi karibuni.
Alisema CCM imefanya kazi kubwa katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi, ambapo kuna ongezeko la wahitimu wa vyuo vikuu.
Katibu Mkuu alisema wakati Rais Jakaya Kikwete, anaondoka madarakani idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu itafikia 200,000.
Alisema serikali imejipanga kukabiliana na tatizo la uhaba wa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali na kwamba, dawa za serikali zitagongwa nembo maalumu ili kudhibiti wizi.
KAMPENI ZA KISTAARABU
Awali, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema CCM itaendelea na kampeni za kistaarabu.
Hata hivyo, alisema waliozoea fujo wakithubutu kufanya hivyo hawatavumiliwa.
“Tunajua ni wasindikizaji lakini katika kusindikiza wakitufanyia fujo watakiona cha mtema kuni lakini tumejipanga kufanya kampeni za kistaarabu,” alisema.
Alisema CHADEMA imeanguka na kilichobaki ni kufanya hitima na kwa kuwa haijajua anguko lake linatokana na nini, itaendelea kushindwa.
Nape alimuahidi Kinana kwamba, Aprili 7, mwaka huu, atampelekea zawadi ya ushindi wa CCM jimboni humo kwa asilimia zaidi ya 90. Uchaguzi utafanyika Aprili 6.
Alisema Ridhiwani anakubalika, hivyo hakuna shaka ya kutwaa jimbo hilo kwa kuwa ni la CCM.
KAULI YA MAMA SALMA
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Wilaya ya Lindi Mjini, na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, alisema Ridhiwani ni kijana mwenye maadili, hivyo anatosha kuwa mbunge wa Chalinze.
“Nimekuja kwa kofia mbili, kwanza mzazi, maana chereko na mwenye mwana, Ridhiwani mwanangu amelelewa ni kijana mzuri mwenye maadili.
“Pili ni MNEC wa Lindi Mjini, ndugu zangu, CCM ndiyo Chama. Msijaribu kuonja sumu kwa kuwa haionjwi, mchagueni Ridhiwani awe mbunge wa Chalinze, mpeni ushindi wa kishindo,” alisema.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, alimnadi Ridhiwani akisema ni kijana aliyelelewa kwenye maadili, hivyo hana shaka.
Aliwasihi wafugaji wa asili ya kimasai wamchague Ridhiwani kwa kuwa anayetafutwa ni mbunge na si kiongozi wa kimila.
“Hapa tunafanya kampeni ya kumchagua mbunge si kiongozi wa kimila, hivyo msihadaike na mgombea wa CHADEMA kwa kuwa hatoshi ubunge, labda kiongozi wa kimila,” alisema.
Sendeka akiimba taarabu, alisema Ridhiwani ni kada aliyeiva na anatosha kuwa mbunge wa Chalinze.
Meneja wa Kampeni, Steven Kazidi, ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, alisema Ridhiwani ni biashara inayouzika, hivyo ushindi ni jambo la uhakika.
Alisema Ridhiwani ni kiongozi aliyeanzia Chipukizi, akawa kiongozi wa UVCCM katika ngazi mbalimbali za mkoa na taifa na sasa ni MNEC, hivyo ana historia katika Chama.
Imani Madega, ambaye alishindwa na Ridhiwani katika kura ya maoni ndani ya Chama, alisema kura hazikutosha na sasa wafuasi wake na wana-CCM wakipiganie Chama.
“Kura hazikutosha, uongozi unapangwa na Mungu, nimegombea mara tatu jimbo la Chalinze lakini sikushinda kwa kuwa Mungu hajapenda, hivyo tumuunge mkono Ridhiwani, tuondoe vinyongo tukunjue nyoyo, tukipiganie Chama,” alisema.
RIDHIWANI ALONGA
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, uliohudhuriwa na umati, Ridhiwani aliahidi neema kwa wananchi wa Chalinze.
Aliahidi endapo atashinda ubunge, jambo la kwanza atakalofanya ni kuhakikisha Shule ya Msingi Machala, iliyoko kata ya Mkange, inajengwa upya kutokana na kutokuwa na hadhi, kwa kuwa ina darasa lililojengwa kwa udongo na kuezekwa nyasi.
Kwa kushirikiana na wananchi alisema kutawekwa utaratibu wa mpango bora wa matumizi ya ardhi ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Tutatenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafugaji na wakulima ili kila upande uweze kuendesha shughuli zake katika mazingira salama bila migogoro,” alisema.
Ridhiwani alisema wafugaji katika mikutano yake ya kampeni wamempa cheo cha Oleogwanan, ambacho anaamini atakitumia kukaa pamoja nao kutatua changamoto hiyo.
Aliahidi atahakikisha anavalia njuga suala la afya ya uzazi kwa kinamama na watoto, kwa kuboresha huduma za afya kwenye zahanati na vituo vya afya.
000
Wednesday, 19 March 2014
Kinana awasha moto Chalinze
09:25
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru