NA FURAHA OMARY
WAKILI Juma Nassoro anayemtetea Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, ameiomba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kutupilia mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), dhidi ya maombi ya marejeo yake.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, kinakataza mtu kuwasilisha maombi yoyote ya marejeo ambayo yanatokana na uamuzi au amri ya mahakama ya chini ambao haumalizi kesi.
Mawakili hao walidai hayo walipokuwa wakiwasilisha hoja za kisheria kuhusu pingamizi la awali la DPP, dhidi ya maombi ya marejeo ya Sheikh Ponda juu ya uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, uliokataa kumfutia shitaka la kukiuka amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Awali, Kongola alidai maombi hayo yanakiuka kifungu hicho ambacho kinakataza kabisa kufanya marejeo kwenye mapingamizi ya awali ya mahakama za chini au katika uamuzi wowote ambao haumalizi shauri.
“Kumbukumbu za mahakama zinaonyesha hoja yao ya msingi wanahoji uwepo wa shitaka la kwanza kati ya matatu ambayo yaliwasilishwa na upande wa Jamhuri dhidi ya mleta maombi (Ponda). Kutokana na tafsiri yao walidai shitaka limefunguliwa kimakosa Morogoro, kwa usahihi lilipaswa kufungulia Kisutu ambako ilitolewa amri,” alidai.Wakili huyo alidai uamuzi wa Mahakama ya Morogoro haukufanya shauri hilo kufikia mwisho bali liendelee na kwamba haukuathiri kufanya shauri kufikia kikomo.
“Tunaomba maombi haya yatupiliwe mbali kwa kuwa yanakinzana na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai,” aliomba.Akijibu hoja hizo, Wakili Nassoro aliiomba mahakama ione hoja za upande wa Jamhuri hazina msingi wowote dhidi ya maombi hayo.
Nassoro alidai Sheikh Ponda si wa kwanza kuwasilisha maombi ya marejeo wakati shauri linaendelea, huku akitolea mfano maombi ya Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph ambao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya ugaidi katika Mahakama ya Kisutu.
Alidai hoja yao ya msingi ni mamlaka ya Mahakama ya Morogoro kushughulikia kosa la kwanza katika hati ya mashitaka na kwamba uamuzi huo ulikuwa unaathiri haki ya Sheikh Ponda ya kushitakiwa katika mahakama isiyo na mamlaka.
“Tunaomba mahakama itupilie mbali pingamizi la awali la upande wa Jamhuri kwa kuwa limekusudia kuona Sheikh Ponda hasikilizwi juu ya uhalali wa kesi iliyoko Mahakama ya Morogoro kabla ya kesi haijaisha,” aliomba.Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Mwarija alisema atatoa uamuzi wa pingamizi hilo la awali Machi 18, mwaka huu.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru