NA CHARLES MGANGA, DODOMA
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Said Nkumba, nusura achafue hali ya hewa bungeni, alipoomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta.
Nkumba katika mwongozo wake jana, alisema wakati wa kupitisha Kanuni za Bunge, mjumbe wa Kamati ya Kanuni, Ismail Jussa Ladhu, alitoa kauli aliyodai inaweza kusababisha mifarakano.
Alisema Jussa alipofafanua michango ya wajumbe wakati wa mjadala wa kanuni, aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar wasiwe na wasiwasi kuhusu maslahi yao.
“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba mwongozo, kuna uhalali wa Jussa kuendelea kuwa mjumbe wa Kamati ya Kanuni na kutupa semina, wakati alitoa kauli nzito inayoweza kuleta mfarakano?
“Nawaomba wajumbe wenzangu waniunge mkono kwa kutokuwa na imani na Jussa, aondolewe kwenye kamati ataleta mifarakano Zanzibar na Tanzania Bara, hana sifa,” alisema.
Sitta alisema kama maneno hayo yaliwakwaza baadhi ya watu, hayamuondolei sifa ya kuwa mjumbe wa Kamati ya Kanuni na kutoa elimu kwa wajumbe kuhusu kanuni.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Profesa Costa Mahalu, alisema wamefanya kazi na Jussa, hivyo ana mchango mkubwa na kwamba, kauli yake ilionyesha hisia za namna mvutano ulivyokuwa wakati wa kutunga kanuni hizo.
“Naomba nikutoe wasiwasi mheshimiwa mjumbe kuhusu suala la Jussa. Aliyosema zilikuwa hisia zake kwa namna hali ilivyokuwa kwenye kamati tulipokuwa tunaandaa kanuni,” alisema.
Profesa Mahalu alisema kwenye semina wao wametumika kama wataalamu wa sheria na si wajumbe wa Kamati ya Kanuni kwa kuwa kamati hiyo iliyoteuliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho, ilimaliza kazi yake.
“Hapa tumetumika kama wataalamu wa sheria si Kamati ya Kanuni. Kwa pamoja tunauthamini ushiriki wa mtaalamu mwenzetu Jussa, ningependa tuendelee kufanya naye kazi,” alisema.
Profesa Mahalu awali, alisema semina hiyo itajikita katika mambo makuu matatu, ambayo ni elimu ya kanuni na matumizi yake, hususan kundi la wajumbe 201 walioteuliwa na Rais, ambao hawana uzoefu na shughuli za bunge.
Mengine ni wajumbe kujua haki zao, hususan wanapokuwa ndani au nje ya bunge na jinsi mjumbe anavyopaswa kutimiza wajibu wake akiwa bungeni.
Wataalamu wengine wa sheria katika semina hiyo ni Evord Mmanda, Tundu Lissu, Amon Mpanju na Dk. Tulia Ackson.
0000
Wednesday, 19 March 2014
Nkumba amvaa Jussa
06:50
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru