Wednesday, 26 March 2014

Bunge lachafuka


Mohammed Issa na Theodos Mgomba, Dodoma

HALI ndani ya Bunge Maalumu la Katiba ilichafuka jana, huku baadhi ya wajumbe wakitaka kupigana baada ya Tundu Lissu, kuwasilisha waraka usiohusu masuala ya bunge kwa siku hiyo.
Lissu aliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, na kutoa waraka aliodai ulitaka kuwasilishwa mbele ya wajumbe na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Ameir Kificho.
Baada ya kusimama, Lissu alionyesha waraka aliodai ni takataka na haufai kujadiliwa, maneno ambayo yaliwaudhi baadhi ya wajumbe.
Waraka huo uliibua maneno kwa baadhi ya wajumbe, ambao walitaka aeleze ameupata wapi.
Wajumbe: Sema umepata wapi waraka huo, sema tueleze mbona sisi hatuna.

Lissu: Mwambieni Mwenyekiti (Sitta), awape, anao.
Malumbano hayo yalisababisha baadhi ya wajumbe kuongea kwa sauti, ndipo Sitta aliposimama na kusema: “Ndugu wajumbe, tuhuma dhidi ya Mwenyekiti wa Bunge ni nzito sana na zinaelekezwa kwake wala yeye hahusiki.”

Alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni ndiye anayeweza kupeleka marekebisho yanayohusu kanuni.

Baada ya Sitta kueleza hayo, Abdallah Bulembo, alisimama na kuomba mwongozo.
Bulembo:  Sisi ni watu wazima, kanuni ndiyo zilizotuleta humu, vikao vya kuzomea haviwezi kuwasaidia Watanzania. Kama vikao vya UKAWA ndiyo hivyo, ni vyema wasiotaka kuendelea na mchakato huu waondoke watupishe sisi tuendelee.

Wajumbe: Haondoki mtu hapa, heee heee heee.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Othman Masoud Othman, alisema bunge linaendeshwa kwa kanuni, haiwezekani mtu mmoja akapitisha mambo peke yake.

Alisema kama ana hoja ya kubadilisha kanuni afuate kifungu cha 87, vinginevyo haitawezekana.
Othman alimtaka Sitta kukataa kuburuzwa na kwamba, bunge linaongozwa kwa kanuni.
Kauli hiyo iliwafanya wajumbe kulipuka kwa furaha, huku wengine wakipiga kofi kwenye meza.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Fredrick Werema, alisema:
“Mambo yote yatafanywa kwa maridhiano ambayo yanataka tufuate kanuni.”

Wajumbe walizomea na kumfanya Jaji Werema kusema, nimeshazoea kuzomewa, nilikuwa mwalimu nilifundisha elimu ya msingi mpaka chuo kikuu.

Jaji Werema alisema waungwana ni vyema wakafuata kanuni ya 87 (i), ambayo inasema Bunge Maalumu linaweza kuzifanyia marekebisho au mabadiliko kanuni zitakazowasilishwa kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu.

Baada ya kauli hiyo, wajumbe walipiga kofi, ambapo Jaji Werema alisema: “Sijazoea kupigiwa kofi nikizungumza.”

Jussa Ismail Ladhu, alisema majukumu ya kamati ya uongozi ni kujadili na kupanga ratiba za Bunge Maalumu la Katiba, ambapo hadi sasa hazijapangwa.

Alisema kamati ya uongozi haina sababu ya kushughulikia Kanuni za Bunge Maalumu.
Sitta alisema migogoro yote ya kanuni huamuliwa na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
Alisema tuhuma zilizotolewa na wajumbe ziwasilishwe kwenye kamati hiyo.
Mwenyekiti Sitta alisema shughuli iliyokuwa ifanyike haitaendelea.
Baada ya kauli hiyo, baadhi ya wajumbe walinyoosheana vidole kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa kuzorotesha shughuli za bunge.

SITTA ALONGA

Baadaye Sitta akizungumza na waandishi wa habari alisema imebainika kuna kikundi cha watu wachache kilichojipanga kuharibu mchakato wa katiba mpya.


Alivitahadharisha vikundi hivyo kuwa ghiliba na hujuma wanazotaka kufanya kukwamisha mchakato huo zimeshabainika.
“Nipo imara, ingawa kazi hii ni ngumu, lakini nawaomba wananchi waelewe kuwa hawa wenzetu hawana nia ya kutufikisha kule tunakotarajia,” alisema.

Sitta alisema vurugu zinazoendelea kufanywa bungeni ni matunda ya  maazimio ya baadhi ya mikutano iliyofanywa mfululizo na kikundi cha  Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA).

Alisema baadhi ya maazimio ya umoja huo, ambao chimbuko lake ni vyama vya upinzani ni mkakati wa kutoka ndani ya bunge na kuhakikisha wanakwamisha kila kitu kinachowasilishwa.
“Si hilo tu, bali wenzetu hawa katika maazimio yao walishapanga kuwa kama maslahi ya UKAWA hayatatimizwa na mwenyekiti wa Bunge hili, hakuna kitakachofanyika mpaka kieleweke, sasa hii ni nini,’’ alihoji.

Alisema UKAWA wanadai Kamati ya Uongozi lazima ifumuliwe, jambo ambalo ni dalili ya kutaka kutofikia mwisho mwema wa mchakato wa katiba.

“Nashangaa, wenzetu hawakujitokeza kugombea nafasi za kuongoza kamati, aliyejitokeza ni Profesa Lipumba pekee na alishindwa na mama Anna Abdallah, sasa CCM imeshinda, wanaanza kuleta siasa za vurugu, hatutafika.


“Kwa utaratibu wa mabunge mengine kuwepo kwa vikundi kama hivyo si jambo baya, kama nia ni kushauriana katika kupata mambo mazuri lakini, kwetu imekuwa kinyume,” alisema.

Alisema tuhuma alizotupiwa na Tundu Lissu, hazikumtendea haki kwa kuwa ni kauli za wongo na uzushi, ambazo zinawapotosha wananchi.

Hata hivyo, alisema kauli za Lissu kamwe haziwezi kumkatisha tamaa ya kufanya kazi hiyo adhimu ya Watanzania.
Alisema ameshapeleka malalamiko kwenye Kamati ya Kanuni ili kuangalia ukweli wa tuhuma hizo dhidi yake.
Kuhusu waraka uliodaiwa kutaka kubadili kanuni ndani ya Bunge uliotolewa na Lissu, alisema haukupangwa kwenye kazi za bunge za jana jioni.
Alisema inashangaza kuona mjumbe huyo alichukua wapi nyaraka ambayo Kamati ya Uongozi ilitoa kwenda Kamati ya Kanuni, lakini kabla haujafanyiwa kazi, aliuchukua na kuuleta bungeni akidai kuwa ni kazi ambazo zipo katika orodha ya jana.
Hata hivyo, Sitta alikiri kuwa kuna kanuni ambazo kamati imebaini zina kasoro na zinapaswa kufanyiwa marekebisho na si zile zilizosomwa na Lissu bungeni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru