- Wananchi washindwa kusafiri
- Stendi yageuka uwanja wa soka
Na Rodrick Makundi, Moshi
USAFIRI katika mji wa Moshi na maeneo ya pembezoni, jana zilisimama kutwa nzima baada ya wasafirishaji kugoma kutoahuduma kwa madai ya kunyanyaswa na askari wa usalama barabarani.
Mgomo huo ulianza jana alfajiri, baada ya wamiliki wa mabasi hayo kuyafungia, hali iliyosababisha kituo cha mabasi cha mjini Moshi kubaki wazi kwa muda wote wa mgomo.
Baadaye, madereva na makondakta wa mabasi, waligeuza kituo hicho kuwa uwanja wa mchezo wa mpira wa miguu, kitendo kilicholazimu jeshi la polisi kuingilia kati.
Hatua hiyo ya jeshi la polisi ilidaiwa kuibua vurugu zilizosababisha gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop, lenye namba za usajili T743 ADC, kurushiwa mawe na kusababisha kioo cha nyuma kuvunjika.
Chanzo cha mgomo huo kilidaiwa ni baada ya madereva kupinga kitendo cha askari wa usalama barabarani kuwakamata na kuwatoza faini kuokana na makosa mbalimbali, bila kuwapatia stakabadhi.
Mgomo huo uliwafanya abiria waliokuwa wanafanya safari zao kwenda katika wilaya zote za Kilimanjaro na mkoani Arusha kukwama kwa takribani kutwa nzima huku wakishuhudia mpira wa miguu uliokuwa unachezwa kituoni hapo na madereva na makondakta hao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, madereva hao walisema kitendo hicho kinaashiria rushwa na kwamba fedha zinazotozwa hazifiki kunakohusika, badala yake kuishia mikononi mwa wajanja wachache.
Madereva hao waliwatuhumu baadhi ya maofisa wa polisi mkoani Kilimanjaro kwa kufanya mambo kinyume cha taratibu, hivyo kuchochea mgomo huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wasafirishaji katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (AKIBOA), Hussein Mrindoko, alidai kuwa kitendo cha baadhi ya askari kugoma kutoa stakabadhi wanapotoza faini, limekuwa jambo la kawaida.
Mrindoko alisema wamiliki wa magari ya abiria wamekuwa wakiumizwa na faini zinazotozwa kwa zaidi ya mara tatu kwa kutwa kitendo ambacho kimegeuka kuwa mtaji kwa baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Kilimanjaro.
Kutokana na mgomo huo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alilazimika kuitisha kikao cha dharura na wadau wa usafirishaji pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama.
Kwenye kikao hicho, baadhi ya maofisa wa polisi waliokuwa wakituhumiwa, walijitetea kwa baadhi ya makosa waliyotuhumiwa nayo, akiwemo mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Kilimanjaro, kudai kwamba alichukua hatua ya kumpiga mmoja wa wamiliki wa mabasi baada ya kutokea hali ya kutoelewana.
Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi katika Kituo Kikuu cha Mabasi Moshi, Henry Nguvumali, alipinga madai ya madereva na wamiliki wa mabasi ya abiria yaliyotolewa kwa mkuu wa mkoa dhidi yake.
Mkuu huyo wa kituo, alituhumiwa kuwa mlevi aliyepitiliza na kwamba amekuwa akifanya mambo yasiyoendana na maadili ya jeshi la polisi ikiwemo kujisaidia ovyo nyuma ya mabasi bila kujali umati mkubwa wa watumiaji wengine wa kituo hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema wadau wote wanapaswa kuzingatia sheria kwenye majukumu yao ya kazi na kuahidi kuchukua hatua dhidi ya askari waliobainika kukiuka maadili ya kazi na kutenda mambo kinyume cha taratibu.
Gama kwa upande wake, aliwasihi wamiliki wa mabasi ya abiria kurejesha huduma kwa kuzingatia kwamba kitendo cha kugoma kimeathiri uchumi wa watu na mkoa kwa jumla.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffari Michael, alisema kushindwa kutoa huduma za usafiri katika kituo hicho kumeisababishia hasara halmashauri hiyo. Alisema Manispaa imekuwa ikikusanya sh. milioni 25 kwa mwezi hivyo, mapato hayo yatapungua.
Tayari Gama ameagiza SUMATRA kuandaa utaratibu wa vikao vya mara kwa mara vya wadau wa usafirishaji kwa ajili ya kuzikabili changamoto zinazojitokeza yakiwemo malalamiko ya wadau
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru