- Sitta ashukiwa ukiukwaji kanuni
- Kamati ya Uongozi kaa la moto
- Profesa Lipumba asusa uteuzi
NA LILIAN TIMBUKA, DODOMA
Wengine wanapinga uamuzi wake wa kutaka kujadiliwa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, ya ufunguzi wa bunge na iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Wakizungumza baada ya kuahirishwa kikao cha bunge jana, walidai Sitta amekiuka kanuni kwa kutenga muda na kuruhusu hotuba hizo zijadiliwe bungeni.
Evord Mmanda, aliyekuwa mjumbe wa kamati iliyoandaa Kanuni za Bunge, alisema hazijaonyesha kipengele kinachoruhusu kujadiliwa kwa hotuba hizo, badala yake zinapaswa kutumika kwa mwongozo katika kupatikana katiba bora.
“Rais alipohutubia bunge kanuni iliruhusu, Jaji Warioba naye alihutubia kwa kufuata kanuni. Ni kanuni gani inaonyesha bunge linaweza kuzijadili hotuba hizo, lazima tufuate kanuni, tusitake kupoteza muda kwa mambo ambayo hayajapitishwa kisheria,” alisema.
Abdallah Bulembo, alisema kwa wajumbe kutaka kushinikiza kujadiliwa kwa hotuba hizo ni sawa na kumkejeli kiongozi mkuu wa nchi, ambaye ndiye aliyewateua.
Bulembo alisema wanaotaka kushinikiza hotuba hizo zijadiliwe wana lao jambo, na hawana nia ya kuwatendea haki Watanzania wanaowawakilisha.
“Rais ndiye aliyetuteua na alikuja kutupa mwongozo wa kufanya kazi ya kutunga katiba. Alitupatia busara kwa kutuongoza wapi tunapaswa kupita, leo tunakuja na hoja ya kutaka kujadili kwa kukosoa kile alichokielekeza, huu ni sawa na utovu wa nidhamu,” alisema.
Hamis Dambaya, alisema haoni dhana ya kutaka hotuba hizo zijadiliwe na kwamba, kufanya hivyo ni kupoteza muda.
“Rai yangu kwa wajumbe ni kuwa, huu muda wa kutaka tuanze kujadili hotuba ni vyema ukatumika kufanya mambo mengine yaliyotuleta hapa,” alisema.
Dk. Ave -Maria Semakafu, alisema hotuba hizo zinapaswa kutumika kama nyenzo ya kufanyia kazi katika majadiliano.
“Rais Kikwete alishatuambia wazi kuwa, yale yalikuwa mawazo yake na akaasa akili zetu tuchanganye na za wengine ili tupate majibu sahihi ya nini kifanyike na uamuzi gani tuufikie,” alisema.
UTEUZI KAMATI YA
UONGOZI MOTO
Wakati huo huo, uteuzi wa majina ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi uliofanywa na Sitta ulizua tafrani na kusababisha Profesa Ibrahim Lipumba, kugomea uteuzi wake.
Baadhi ya wajumbe walioomba mwongozo baada ya Sitta kutaja majina ya wajumbe watano aliowateua, walilalamika kuwapo upendeleo katika uteuzi.
Walioteuliwa kuungana na wenyeviti wa kamati zingine kuunda Kamati ya Uongozi iliyoanza kazi jana ni Fakharia Hamis Shomari, Mary Chatanda, Amon Mpanju, Profesa Lipumba na Hamad Abuu Jumaa.
Mohamed Habib Mnyaa, alisema uteuzi huo haukuzingatia uwiano, ikizingatiwa hoja inayotarajiwa kuteka mjadala wa bunge ni ya Muungano, ambao unalalamikiwa na Wazanzibari.
“Kama katika Kamati ya Uongozi, ambayo ndiyo inatengeneza ajenda za kuja kujadiliwa ndani ya bunge ina Wazanzibari watano kati ya wajumbe 19, unatarajia kuna haki itatendeka hapo, mwenyekiti hujatutendea haki,” alisema.
PROFESA LIPUMBA
ASUSA UTEUZI
Profesa Lipumba alisema suala la uwakilishi wa Zanzibar ndani ya bunge katika kila nyanja ni la muhimu.
“Naona CCM mmejipanga vyema kutumaliza, Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa uteuzi wako lakini natangaza siko tayari kukubali uteuzi huu, naomba jina langu liondolewe,” alisema.
Alisema hakubali uteuzi huo, ambao alidai unalenga kumfanya aonekana kutumiwa na CCM kwenye uamuzi wa kila jambo, hivyo anawaachia walioteuliwa waendelee na kazi na yeye atabaki kuwa mjumbe.
“Nasubiri tuje tupambane huku ndani kwa hoja,” alisema.
John Mnyika, alisema uteuzi umekosa sura ya uwiano wa pande zote za Muungano na wa makundi mbalimbali.
Alisema kamati hizo zitaendelea kulalamikiwa kwa kuwa CHADEMA imekosa wawakilishi.
SITTA AJIBU MAPIGO
Mwenyekiti Sitta alisema uamuzi wake hauwezi kumfurahisha kila mtu ndani ya bunge.
“Kwa mfano Fakharia, ametoka Zanzibar, Lipumba ametoka CUF, sasa mlitaka nifanyeje zaidi ya hapo, wakati kanuni inanitaka nizingatie uwiano, jinsia na makundi mbalimbali ya uwakilishi, na ndicho nilichofanya,” alisema.
Valerie Msoka, akizungumza nje ya ukumbi wa bunge alisema kila mjumbe alipewa uhuru wa kugombea lakini baadhi hawakufanya hivyo na sasa wanalalamika.
“Kama mjumbe hakujitokeza kugombea asilalamike, kwa kuwa demokrasia imefuatwa na watu hawakutaka kujitokeza. Ifike mahali tutambue tuko hapa kwa ajili ya nini, badala ya kuendelea kusikiliza malalamiko kila siku, hatutafika,” alisema.
Alisema bunge limetawaliwa na siasa za vyama na ubinafsi, ambao hauwezi kumkomboa Mtanzania.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru