Monday, 17 March 2014

Mgimwa apeta



  •  Aongoza kata 11 kati ya 13, utulivu watawala
  •  Wafuasi CHADEMA wakamatwa na silaha
  •  Chopa yake yasuswa na wananchi

NA waandishi wetu, KALENGA
MGOMBEA ubunge Kalenga kwa tiketi ya CCM, Godfrey Mgimwa, anaongoza kwa kura katika kata 11 kati ya 13 za jimbo hilo.

MGOMBEA wa CCM katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa, akizungumza na
waandishi wa habari baada ya kukagua vituo vya kupigia kura katika uchaguzi huo uliofanyika jana. (Na Bashir Nkoromo).


CCM inaongoza katika kata za Rumuli, Kalenga, Kiwere, Mgama, Ifunda, Wassa, Mseke, Mangalila, Maboga, Ulanda na Lushota.
Wananchi walijitokeza kwa wingi jana asubuhi kupiga kura kwa amani na utulivu, licha ya kauli za vitisho kutoka kwa wanasiasa.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja asubuhi na muda mfupi baadaye kulikuwa na misururu mirefu ya wapiga kura.
Umati ulijitokeza katika vituo vya Kalenga Mjini, kata ya Kalenga na Mangalila, kata ya Ulanda.
Katika kata ya Maboga, vituo vilifunguliwa kwa wakati, ambako wapiga kura wa rika zote walijipanga kwenye mistari kwa utulivu wakisubiri kupiga kura.
KAULI ZA WAPIGA KURA
Onesmo Makasi, mkazi wa Mangalila, akizungumza baada ya kupiga kura, alisema alifika kituoni saa 1.30 asubuhi na kukuta kila kitu kikiwa kimeandaliwa, hivyo alipiga kura kwa urahisi.
Makasi alisema awali alihisi uchaguzi  ungegubikwa vurugu kutokana na kauli zilizotolewa na baadhi ya wanasiasa lakini hali ilikuwa tofauti.
“Nimepiga kura kwa amani na utulivu. Kutokana na mazingira haya naamini mshindi atatangazwa mapema,” alisema.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Zaina Konzi, alisema amefurahi kupiga kura kwa amani na utulivu.
Kutokana na hilo, aliipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha upigaji kura unafanyika kwa amani.
ULINZI WAIMARISHWA
Katika kipindi chote cha upigaji kura, ulinzi uliimarishwa vituoni, Jeshi la Polisi likiwa limejipanga kutokana na askari kuwepo kwenye vituo vya kupiga kura.
Katika kata zote na vijiji vya Kalenga, askari polisi walikuwepo kulinda usalama.
Askari ambaye hakupenda kuandikwa jina gazetini, aliyekuwa kituo cha Kalenga A na Kalenga B, alisema wamejipanga kulinda amani na hapakuwa na viashiria vya kuivuruga.
HELIKOPTA YA CHADEMA
CHADEMA iliyoshikilia msimamo wa kutumia helikopta maarufu Chopa, iliitumia kuzunguka kwenye kata mbalimbali, zikiwemo
Kalenga, Nzihi, Ifunda na Wassa.
Hata hivyo, wananchi waliokuwa kwenye misururu ya kupiga kura, hawakuikimbilia kuishangaa, badala yake walibaki kwenye foleni kuhakikisha wanatimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
Jeshi la Polisi lilizuia matumizi ya helikopta jana ili kuwawezesha wananchi kupiga kura kwa utulivu.
CHADEMA waliondoa nembo ya chama hicho kwenye helikopta hiyo ili kutimiza sheria na kanuni za uchaguzi.
KAULI ZA VITISHO
Kabla ya uchaguzi jana, kauli za vitisho zilitolewa na baadhi ya wanasiasa kwenye mikutano ya kampeni, ambazo ziliwatia hofu wananchi.
Ilielezwa kuna vijana wamefichwa porini ili kuwazuia wananchi wasiende kupiga kura. Vyama vya siasa vilishutumiana kwa kupanga kuharibu uchaguzi huo.
Miongoni mwa kauli hizo ni uwepo wa makundi ya vijana walioingia Kalenga kwa ajili ya kufanya vurugu.
Baadhi ya wanasiasa waliwahamasisha wafuasi wao kujiandaa kwa mapambano endapo matokeo yatakayotangazwa hayatakuwa mazuri kwa upande wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi, alionya atakayethubutu kufanya vurugu atakiona cha moto.
Alisema polisi wamejipanga kukabiliana na kila aina ya hila na visa ambavyo vinaweza kuvuruga uchaguzi.
Hata hivyo, imeripotiwa baadhi ya vijana wa CHADEMA walitaka kufanya usumbufu kwa kuzuia wapiga kura, hususan wanawake katika eneo la Ibumilla, kata ya Mgama, lakini walidhibitiwa na vyombo vya usalama.
SILAHA ZAKAMATWA
Vijana wawili wanaodaiwa wafuasi wa CHADEMA wanashikiliwa polisi wakituhumiwa kukutwa na visu, mikuki na nondo.
Akizungumza na waandishi wa habari,  Kamanda Mungi alisema baada ya kupekuliwa vijana hao pia walikutwa na bendera ya CHADEMA.
Kamanda aliwataja vijana hao kuwa Walter Wanuo (37), mkazi wa Mianzini, Arusha na Edward Julius (26) wa Namanga, Arusha.
Alisema silaha hizo za jadi zilikuwa ndani ya gari aina ya Toyota Prado namba T 808 AMX. Pia kulikuwa na mawe 37, fimbo nane, mipira 13, virungu vitatu na visu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru