Tuesday 18 March 2014

‘Fikirieni mbadala wa kujikwamua kiuchumi’


NA WILLIAM SHECHAMBO
WAAMINI wa dini ya Kiislamu nchini, wametakiwa kufikiria mfumo mbadala utakao wasaidia kujikwamua kiuchumi, unaozingatia mafundisho ya dini hiyo.


Hatua hiyo inalenga kuzitambua fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo yanayowazunguka na kuzitumia, ili ziwaletee tija.
Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la siku mbili linalofanyika katika ukumbi wa Kariamjee, Dar es Salaam, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ally Hassan Mwinyi, alisema umefika wakati kwa Waislamu kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo ili wajikwamue kiuchumi.
Mwinyi ambaye pia ni Mlezi wa Jumuiya ya Wasoma Quran Tanzania (JAWAQUTA), alisema Waislamu wengi ni waoga wa kujaribu kufanya kitu kinachoweza kuwaletea maendeleo.
Aliwataka wanazuoni na masheikh wanaohudhuria kongamano hilo, watumie muda huo kutathmini ili wapate suluhisho la kudumu la namna ya kujikwamua kiuchumi kupitia taasisi za kifedha za serika na binafsi.
“Serikali yetu ni sikivu, mtakalokubaliana kuhusu mustakabali wa mfumo wa kukuza uchumi kwa wananchi, bila shaka itayachukua mawazo hayo na kuyafanyia kazi,” alisema Rais Mwinyi.
Naye Mwenyekiti wa JUWAQUTA, Shekhe Mussa Salum, alisema tatizo linalowakabili waislamu ni riba katika taasisi za fedha.
Alisema riba katika mafundisho ya Kiislamu ni haramu, hawapati nafasi ya kupata mikopo kutokana na masharti hayo, isipokuwa kwenye benki chache zenye dawati kwa ajili ya miamala ya Kiislamu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru