NA SULEIMAN JONGO, IRINGA
MGOMBEA ubunge wa CCM, katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Godfrey Mgimwa, ameanza kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ucheleweshwaji wa mbolea.
Godfrey Mgimwa |
Alitoa kauli hiyo jana, katika kijiji cha Usengelindete, kata ya Wassa, wakati akiomba kura kwa wananchi ili aliongoze jimbo hilo na kuliletea maendeleo.
“Ndugu zangu naomba nichagueni ili niweze kushughulikia suala la mbolea ambalo linalalamikiwa kutokana na kutofika kwa wakati. Tayari nimeanza kutafuta ufumbuzi na iwapo mtanichagua naahidi kufanya kazi kwa kikamilifu,” alisema Mgimwa.
Alisema anatambua shughuli za kilimo katika jimbo hilo na mkoa wa Iringa kwa ujumla ndizo zinazopewa nafasi katika kukuza uchumi, hivyo moja ya mambo atakayofanya ni kutengeneza mazingira bora ya kilimo cha kisasa.
Akizungumzia suala la maendeleo, Mgimwa aliwahakikishia wananchi kuwa endapo atachaguliwa atakuwa tayari kutumwa na kufanya kazi zitakazoharakisha maendeleo.
Kwa mujibu wa Mgimwa, tayari ana mwongozo wa kumuwezesha kufanya kazi za kibunge jimboni humo.
“Niko tayari kutumwa, wazee wangu, vijana wenzangu na wananchi wote wa Kalenga, nipeni nafasi niwatumikie. Umri wangu unaniruhusu kufanya kazi yoyote na wakati wowote,” alisema Mgimwa.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru