Wednesday, 26 March 2014

Sefue aridhishwa ujenzi bomba la gesi


NA FURAHA OMARY

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ameelezwa kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoa Mtwara hadi Dar es Salaam.
Amesema miradi huo ni sehemu ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), ambao ulipokuwa ukianza watu walikuwa wakikebehi.



Balozi Sefue aliyasema hayo juzi mjini Dar es Salaam, alipotembelea kituo cha kufua umeme kwa kutumia gesi asilia cha Kinyerezi 1, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku mbili ya kukagua mradi wa ujenzi wa bomba la gesi.
“Baada ya siku mbili kutembelea mradi wa gesi, napenda kuipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kusimamia mradi huo ambao ni sehemu ya BRN. Kuna watu wakati tunaanza walikebehi, lakini tumeona utekelezaji unavyokwenda vizuri na tuna matumaini utakamilika kadri ulivyopangwa.” alisema.
 Katibu Mkuu Kiongozi aliihimiza wizara hiyo kusimamia vizuri mradi huo na makandarasi nao wanapaswa kujua kwamba serikali haitaki mchezo kazi ikitolewa lazima ikamilike kwa wakati uliopangwa.
“Hatuna mchezo lazima kazi ikitolewa ikamilike kwa wakati. Wananchi wameshateseka sana kuhusu umeme kama alivyoagiza Rais ifike mahali tuseme tatizo la umeme sasa basi,” alisema
 Balozi Sefue aliwahimiza makandarasi na wizara hiyo kuhakikiasha kila kitu kinakamilika kwa wakati.
Aidha, aliihimiza wizara hiyo kukusanya uzoefu wa nchi nyingine duniani ambazo ziliwahi kutumia gesi kwa kuwa kuna zilizofanikiwa na zisizofanikiwa ili kujifunza.
Pia alisema gesi ni kichocheo cha uchumi kukua, hivyo lazima kujenga uchumi vizuri kwa sababu ipo siku gesi itaisha na wasimamie vizuri mapato ya gesi ili kuwa na manufaa yatakayodumu.
Balozi Sefue aliwatoa hofu wale wanaodhani wananchi wanaopitiwa na mradi huo hawajanufaika na kuwataka kwenda Mtwara na Lindi kujionea.
Alisema wananchi hao wamenufaika kwa watoto kupewa udhamini na kupata maji safi na ajira mbalimbali. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru