Wednesday, 14 May 2014

Ajali yaua 9, yajeruhi 11


NA PETER KATULANDA, MWANZA
WATU tisa wakiwemo watoto wawili, wamekufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa, baada ya gari la abiria aina ya Toyota Coaster, walilokuwa wakisafiria kugonga roli lililoegeshwa barabarani na kupinduka.
Ajali hiyo mbaya ilitokea juzi saa 1:30 usiku, katika barabara kuu ya Mwanza - Musoma eneo la Nyam’hongolo wilayani Ilemela jijini Mwanza, ambapo Coaster hiyo yenye namba T769 CQE, iligonga tela la roli hilo.
Kwa mujibu wa watu mbalimbali walioshuhudia ajali hiyo, Coster hiyo (Tinsela Express) iliyokuwa na mwendo kasi, ilikuwa ikiendeshwa na dereva aliyetambulika kwa jina la Yohana Mayandakia, kutoka jijini Mwanza kwenda Bunda mkoani Mara.
Baadhi ya madereva waliokuwa wamefuatana na gari hilo, walidai kuwa Mayandakea hakuwa waangalifu na ishara ya roli hilo lenye namba ya usajili T832 AEF aina ya IVECO lenye tela namba T187 AEF, lililokuwa limeegeshwa barabarani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, alisema chanzo chake ni uzembe wa dereva wa Coaster.
Alisema watu tisa wakiwemo watoto wawili, walikufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa vibaya.
Alisema watu wazima waliokufa katika ajali hiyo ni saba (wanaume wanne na wanawake watatu).
Aliwataja marehemu kuwa ni pamoja na  Mwalimu wa Sekondari ya Buhongwa, Angelina Ngusa, Elias Jonas Ndege na wengine waliofahamika kwa jina moja la Hussein na Alex. Mtoto mmoja alifahamika kwa jina la Ester Petro.
Alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Bugando (BMC) na majeruhi wote wamelazwa kwa matibabu.
Muuguzi Msaidizi wa BMC, Eflasia Nyange, aliwataja majeruhi kuwa ni Hamdani Haluna, Nyanda Sahani, Magesa Musa, Shija Nyanda, Rosemary Petro, Priske Peter, Nerhar Ignas, Benson Joseph, Lushinge Nyerere, Mosha John na Japhet Mlagwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru