- Waliotafuna fedha za kuanzisha Family Benki kusulubiwa
Na Mwandishi wetu.
BARAZA Kuu la Jumuia ya Wazazi Taifa linakutana leo mjini Dodoma likiwa na ajenda kuu moja ya kujadili taarifa ya Tume ya Dk. Edmundi Mndolwa, kuhusu kukwama kwa Benki ya Family.
Habari zilisema baraza hilo linakutana leo huku taarifa za tume hiyo ya Dk. Mndolwa, zikiwa ni siri nzito ambayo imewaacha wajumbe wengi wakihaha kutaka kujua nini kimebainika kuhusiana na uanzishwaji wa benki hiyo.
Uchunguzi uliofanya na UHURU WIKENDI umebaini kuwa kukwama kwa benk hiyo kumesababishwa na baadhi ya viongozi waandamizi wa Jumuia hiyo kutumia sh. milioni 200 ambazo zilitolewa na wafadhili wa benki hiyo Kampuni ya Family Finance.
Hata hivyo, matumizi hayo yalikuwa sio ya kiofisi na inadaiwa kuwa baada ya mamilioni hayo kutumika kiholela bila maelezo kamili, wafadhili hao walikwama kuendelea na ari ya kuanzisha benki hiyo.
Pia, imebainika kuwa kupotea kwa fedha za baadhi ya wanachama waliokuwa wa benki hiyo ambao ni watumishi wa jumuiya hiyoni sababu nyingine iliyofanya iundwe Tume ya Dk. Mndolwa.
Baada ya kuwepo kwa sintofahamu juu ya benk hiyo, Wajumbe wa Baraza Kuu lililokutana Februari 20, mwaka huu, waliazimia kuundwa kwa tume hiyo na kutoa siku 60 ili kuitishwa kwa baraza lengo likiwa kujadili taarifa ya tume hiyo.
Kutokana na kutovuja kwa taarifa ya Tume ya Dk. Mndolwa, kumesababisha wajumbe kuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua nini kimejiri katika taarifa hiyo na nini hatma yao kwa wale ambao tayari walishatoa michango kwa ajili ya kuanzisha benki hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi waandamizi wa Jumuia ya Wazazi walipotakiwa kueleza kuhusu mkutano wa leo, walidai wanatekeleza agizo la Baraza Kuu na kuwa hawana cha kujadili zaidi ya taarifa itakayowasilishwa leo na Dk. Mndolwa.
Gazeti hili lilibaini kuwa kutokana na hofu na wasiwasi kuhusu taarifa ya tume, baadhi ya viongozi walijipanga kuvuruga mkutano wa leo kwa kuanzisha malumbano ya ndani kwa ndani.
Akizungumza katika moja ya vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliionya Jumuia ya Wazazi kuwa inaweza kufutwa na Chama wakati wowote.
Akitoa tahadhari hiyo mwaka 2012, Rais Kikwete alisema jumuia hiyo imepoteza mwelekeo, imekosa uhalali na kamwe haina faida yoyote tena kwa Chama na kuwa Kamati Kuu ilijadiliana kwa muda mrefu kama taasisi hiyo bado inastahili iendelee kuwepo ama ifutiliwe mbali na kubaki mbili tu za Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Moja kati ya sababu zilizosababisha jambo hilo lifikiriwe ni jumuia hiyo kushindwa kutimiza wajibu wake wa kisiasa, pia ikashindwa kusimamia hata shule zake zilizokuwa msingi wa kuanzishwa kwake na badala yake kugeuka kuwa vitega uchumi vya wajanja wachache tu.
Alihoji uhalali wa kuendelea kuwepo huku ikiwa mzigo ulioshindwa kubebeka, imegeuka kuwa pango la ufisadi na kuzidi kuikamua CCM kwa kupata mgao wa ruzuku na misaada mingine wakati haina faida yoyote.
Akihitimisha onyo lake, Rais Kikwete alisema baada ya mjadala huo mkali, Kamati Kuu iliamua kutoa muda mwingine kwa Jumuia ya Wazazi, lakini unaweza kuwa wa mwisho endapo itashindwa kabisa kujirekebisha.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru