Friday, 16 May 2014

Jiji Dar latenga sh. milioni 22 kukabiliana na Dengue


NA RACHEL KYALA
TAKRIBANI  sh. milioni 22 zimetengwa na Halmashauri za jiji la Dar es Salaam ili kukabiliana na ugonjwa wa Homa ya Dengue. 
Hadi kufikia Mei 15, mwaka huu, watu 494 walipimwa na kugundulika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo huku Manispaa ya Kinondoni ikiongoza kwa kuwa na wagonjwa 389, Ilala 73 na Temeke 32.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick, alisema hayo jana alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu ugonjwa huo ambapo alisema  wagonjwa wanaendelea kuhudumiwa kwenye hospitali za Amana, Mwananyala, Temeke  na zile za binafsi.
"Shule za msingi na sekondari 40 zimepatiwa elimu kupitia mpango wa elimu shuleni huku takribani majengo 20 zikiwemo ofisi za umma, shule, hospitali, zahanati na vituo vya afya vikiwa vimeshapuliziwa dawa na kazi inaendelea," alisema.
Pia,  alisema lita 940 za dawa aina ya bacillus thringiensis aIsraelensis (Bti) zimenyunyizwa kwenye madimbwi yaliyoko maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam yalioathirika zaidi huku zaidi ya kata 58 zikiendelea kuwekewa viuadudu na kuharibu mazalia ya mbu.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuzingatia usafi wa mazingira ikiwemo kufyeka nyasi, kuondoa makopo, matairi, vifuu  vya nazi na madafu, kufukia madimbwi na kusafisha mitaro ili kuondoa mazalia ya mbu.
Pia aliwataka kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa nguo zinazofunika sehemu mbalimbali za mwili, kupaka dawa ya kufukuza mbu ikiwa lazima kuwepo maeneo hayo huku akiwataka wananchi walioko mabondeni kuondoka kwani ni maeneo hatarishi zaidi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru