- Thamani ya ekari moja ni milioni 141/-
- Ni fidia ya kupisha ujenzi wa mji mpya
NA TUMAINI MSOWOYA, DODOMA
WAKAZI wa Kigamboni, Dar es Salaam, ambao maeneo yao yatachukuliwa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa mji mpya, watalipwa fidia ya shilingi milioni 141.6 kwa ekari moja.
Malipo hayo ni sawa na sh. 35,000 kwa mita moja ya mraba.
Malipo hayo yalitangazwa juzi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alipokuwa akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
"Hiki ni kiwango cha fidia kwa mujibu wa sheria kulingana na thamani ya ardhi iliyopo katika mji huo wa Kigamboni,îalisema Profesa Tibaijuka.
Aliwataka wakazi wa Kigamboni, wasikubali kuuza maeneo yao kwa bei poa kutokana na kuibuka kwa kundi la wajanja linalowarubuni kufanya hivyo.
Waziri Tibaijuka alisema wajanja hao wamekuwa wakiwadanganya wananchi kwa kununua maeneo yao ili baadaye walipwe fidia na Wakala wa Kuendelea Mji wa Kigamboni (KDA).
Alisema serikali imeandaa mpango kabambe wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni kwa kasi katika mwaka huu wa fedha,ikiwemo kufanya tathmini ya mali na kulipa fidia wananchi ili kupisha ujenzi wa mradi huo.
Aliwaonya wale wanaowarubuni wananchi na kununua ardhi yao, kuacha mara moja kufanya hivyo na kuwataka wanaodhani kazi hiyo imeshindikana, kubadili mtizamo wao.
Alisema katika mwaka wa fedha uliopita, wizara yake haikuweza kutekeleza mpango wake wa kuendeleza mji wa Kigamboni, kutokana na ukosefu wa fedha.
"Ninawahimiza wananchi wa Kigamboni kuendelea kuwa wavumilivu na kutokubali kurubuniwa kuuza maeneo yenu kwa wajanja, ambao baada ya viwango vya fidia kutajwa, wamejitokeza wakitaka kununua ardhi zenu kwa bei poa,îalisema
Aliwataka wananchi wa mji huo, kuitambua KDA na kutokubali kudanganywa na wale wanaotaka kupima maeneo ya mji wao bila fidia stahiki kulipwa.
Alisema wananchi wa Kigamboni wataendelea kubaki Kigamboni katika makazi mapya yatakayojengwa katika eneo la Uvumba, kata ya Kibada.
Profesa Tibaijuka alisema wananchi hao watawezeshwa kutumia sehemu isiyopungua asilimia kumi, kununua hisa za KDA kwa lengo la kuendelea kufaidi matunda ya mji mpya wa Kigamboni.
Alisema Machi, mwaka huu, mtaalamu aliteuliwa na ameshaanza kazi yake, jambo ambalo litaongeza kasi ya kuchochea ujenzi wa mji huo mpya. Alisema
watapima maeneo ya miundombinu, umma na kusimamia utekelezaji wa mpango kabambe kupitia KDA.
Aliwataka wananchi wa Kigamboni kuendelea kuwa na imani na mpango huo kwa kwa kuwa hatua iliyofikiwa mpaka sasa ni nzuri.
Aliwaondoa wasi wasi wale wanaodhani kuwa kazi hiyo imeshindikana kwa madai kuwa mradi huo unatekelezwa kutokana na maagizo ya Ilani ya CCM ya mwaka 2010.
Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira,
imeishauri wizara hiyo kuhakikisha kuwa inawashirikisha wananchi katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo.
Akisoma taarifa ya kamati hiyo, Ester Bulaya alisema utekelezaji wa mradi huo umechukua muda mrefu tangu mwaka 2008, kiasi cha kuwakatisha tamaa wananchi.
Aliishauri wizara hiyo kuanza mara moja utekelezaji wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni kwa kujenga miundombinu huku maeneo mengine yakiachwa kwa ajili ya wawekezaji.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru