Wednesday, 14 May 2014

JWTZ: Tuko tayari kwa lolote, tunasubiri amri



  • Laonya haliyumbishwi na kauli za kisiasa
  • Wabunge walia na maslahi ya wanajeshi

NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
JESHI la Wanachi wa Tanzania (JWTZ), limeonya kuwa liko imara na litaendelea kusimamia na kutii amri na maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete.
Pia, limesema kamwe halitayumbishwa na hila na kauli za kisiasa zinazotolewa kwenye majukwaa.
Kauli hiyo ya wapiganaji na walinzi wa taifa ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, wakati akiwasilisha Makadirio ya Matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Alisema Rais Kikwete ni kiongozi shupavu, mvumilivu na mwenye kupenda maridhiano, mambo ambayo yatamfanya akumbukwe na kuenziwa vizazi na vizazi.
“Ahadi yetu kwake ni kuwa tutaendelea kusimama imara kupokea na kutii amri na maelekezo yake bila hila yoyote na kutoyumbishwa na kauli potofu za kisiasa,’’ alisema Dk. Mwinyi.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2014/2015, wizara inakusudia kuimarisha utendaji kazi na ufanisi wa jeshi hilo katika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa taifa kulingana na dira, dhima na malengo.
‘’Mpango wa ununuzi wa zana za kisasa na bora za kijeshi ni endelevu, hivyo natarajia Bunge lako litaendelea kuidhinisha na kutekeleza mpango huu,’’ alisema.
Alisema mpango huo unalenga kuimarisha  mafunzo ya kijeshi kwa vijana kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea.
Dk. Mwinyi alisema mpango huo unalenga kununua vifaa na zana za kijeshi za kisasa, vikiwemo vifaa vya uhandisi wa medani na ndege za kivita na kuendelea na ujenzi wa nyumba  6,064 kwa ajili ya makazi ya wanajeshi.
Aidha alisema hivi sasa vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza kutekeleza utaratibu wa kuajiri vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa.
Alisema katika kipindi cha mwaka huu, vijana 7,062 waliajiriwa na vyombo hivyo huku wengine 155 wakichukuliwa na kampuni binafsi, ikiwemo Benki Kuu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Kampuni za Madini za Barrick na Geita Gold Mines.
Alisema kwa kipindi cha mwaka huu, vijana 45,000 watakaomaliza kidato cha sita watachukuliwa kwa ajili ya mafunzo ya JKT.
Mwinyi alisema utaratibu wa vijana waliomaliza kidato cha sita kujiunga na JKT kwa mujibu wa sheria si wa hiari.
Kwa mujibu wa Mwinyi, awamu ya kwanza kwa mwaka huu itaanza Juni hadi Septemba na itahusisha vijana 20,000 huku awamu ya pili ambayo itachukua vijana 14,450, itaaanza Oktoba hadi Januari, mwakani.
Alisema awamu ya tatu itakayochukua vijana 10,550 itaanza Januari mwakani.
Akizungumzia uvamizi wa maeneo ya jeshi, Dk. Mwinyi alisema tatizo hilo bado kubwa na linaendelea.
Alisema katika kipinchi hiki, maeneo yaliyoathirika na tatizo hilo ni pamoja na Tondoroni (Pwani), Tanganyika Packers na Monduli (Arusha), Kimbiji
(Dar es Salaam), Chita (Morogoro), Itaka na Uyole (Mbeya).
Sehemu nyingine ni Uwanja wa Ndege na Ilemela (Mwanza) na Kisakasaka (Unguja).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru