Tuesday, 20 May 2014

Kampuni, taasisi zatakiwa kufunga CCTV


TAASISI na kampuni binafsi nchini zimetakiwa kufunga vifaa vya kisasa vya kurekodi matukio (CCTV), kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu ili kudhibiti na kuzuia vitendo vya uhalifu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima, alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Kangi Lugola (Mwibara-CCM), aliyetaka kujua sababu za serikali kutofunga vifaa vya kisasa vya CCTV, ambavyo vitasaidia kuzuia na kudhibiti uhalifu hasa katika miji mikubwa.
Silima alisema wakati serikali ikijipanga kusimamia ufungaji wa CCTV kwenye maeneo muhimu, ni vyema kampuni, taasisi na watu binafsi wakaanza kufunga vifaa hivyo kwenye maeneo yao.
Alisema kwa sasa serikali inaendelea kufanya uchambuzi wa mapendekezo ya kibiashara na sekta binafsi ili kuwekeza teknolojia hiyo na miundombinu yake katika kutimiza malengo ya usalama wa nchi.
Alisema ni ukweli usiopingika kuwa ufungaji wa vifaa vya ulinzi vya CCTV  ni muhimu katika kupunguza uhalifu wa aina mbalimbali hapa nchini.
Aliongeza kuwa suala la ufungaji wa vifaa hivyo katika maeneo muhimu ni suala  mtambuka linaloshirikisha wadau mbalimbali, zikiwemo wizara ya miundombinu, mipango miji, serikali za mitaa na watu binafsi.
ìHuu ni mradi mkubwa unaohitaji utafiti wa kutosha wa kimiundombinu, kisheria na raslimali fedha na kwamba wizara inabaki kama msimamizi mkuu wa kzzi za mradi huo katika kudhibiti uhalifu,îalisema.
Kwa kutambua umuhimu huo,  Silima alisema Jeshi la Polisi katika mpango wake wa maboresho, linatekeleza miradi 27 ya ICT, ikiwemo kufuatilia taarifa za usalama barabarani ili kupunguza ajali.
Alisema  ufanisi wa zoezi hilo umekuwa ukikwamishwa kutokana na ufinyu wa bajeti.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru