Thursday, 22 May 2014

Wajasiriamali wa chumvi watakiwa kujisajili


SERIKALI imevitaka vikundi vya wajasiriamali wa chumvi, kujisajili ili kupata mikopo ya masharti nafuu na kujiunga na Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania (TASPA).
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Aggrey Mwanry, alitoa mwito huo jana alipokuwa akijibu swali la
Christina Lissu (Viti Maalumu-CHADEMA).
Mbunge huyo alitaka kujua mkakati wa wizara kuhusu wanakijiji wa kata ya Kikio na Misughaa wilayani Ikungi, wanaojishughulisha na uzalishaji chumvi katika ukanda wa Bonde la Ufa.
Mwanry alisema Halmashauri ya  Ikungi inavyo vikundi viwili vya uzalishaji chumvi, ambavyo ni NGAA Group na ISANJA Group, vilivyoanzishwa mwaka 2007, ambavyo vina jumla ya wanachama 165.
Alisema serikali kwa kutambua umuhimu wa vikundi hivyo, ilivipatia mabomba 30 kupitia uhisani wa UNICEF kwa ajili ya kuchanganya madini joto na chumvi.
Naibu Waziri alisema pia kuwa vikundi hivyo vilipewa madini joto na vifaa vya kupimia madini joto kutoka Tanzania Food $ Nutrition Centre (TFNC) na mafunzo ya jinsi ya kuchanganya chumvi, madini joto na kuhifadhi chumvi isipoteze ubora.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu, Halmashauri ya wilaya ya Singida kabla ya kugawanywa kuwa mbili, ilipata mkopo kwa vikundi 14 vya kinamama wajasiriamali vilikopeshwa sh. 7,000,000 mwaka 2012.
Alisema mwaka 2013/2014, vikundi 19 vya kinamama wajasiriamali vilikopeshwa sh.milioni tisa na mwaka huu, Halmashauri ya Ikungi imetenga sh. 62,800,000 kwa ajili ya mikopo ya masharti nafuu kwa vikundi vya kinamama na vijana.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru