Tuesday, 20 May 2014

Mama Karume naye afunguka


NA ABOUD MAHMOUD, ZANZIBAR
WASOMI nchini wametakiwa kuwa makini na kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa, wanaobeza Muungano na kutaka uvunjike.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume, Mama Fatuma Karume wakati alipokutana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la CCM, nyumbani kwake Maisara mjini Unguja.
Alisema kuna haja ya wanafunzi kujifunza historia ambayo itawasaidia kufahamu kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unatakiwa kudumishwa na kulindwa kwa gharama yoyote.
Mama Fatuma alisema Muungano huo ndio uliosaidia kuwainua na kuwaondoa kwenye manyanyaso wananchi wa Zanzibar.
“Nakuombeni wajukuu zangu, nyinyi ndio wasomi na ndio viongozi wa baadaye, jitahidini kusoma historia ya kweli. Muungano ni kitu muhimu ambacho kimetusaidia na kutukomboa sisi Wazanzibari,” alisema.
Alisema anashangazwa na kauli za baadhi ya watu kudai kuwa, Muungano hauna umuhimu, jambo ambalo alisema linapaswa kupuuzwa.
“Miaka yote wameona Muungano una faida, lakini sasa umetimiza miaka 50, ndipo wanasimama na kubeza na kuona ubaya wake. Tusiwafuate viongozi wa aina hii, tujifunze kuuenzi na kuulinda muungano wetu,” alisema.
Mama Fatuma alisema pia kuwa, Muungano huo haukufikiwa kwa bahati mbaya na kwamba, malengo yake yalikuwa ni kwa manufaa ya watu wake na hilo linathibitishwa na maisha halisi ya sasa.
Alisema Wazanzibari wengi wanaishi kwa uhuru Tanzania Bara na kufanya shughuli bila kubughudhiwa na wamekuwa kitu kimoja.
Mwenyekiti wa UVCCM Tawi la Chuo Kikuu cha Mzumbe, Victor Mhagama, alisema mawazo waliyoyapata na historia waliyoipata kutoka kwa Mama Fatuma na viongozi wengine wa CCM, imewasaidia kufahamu zaidi umuhimu wa Muungano.
Naye Katibu wa UVCCM, Nicodemus Kasebwa, alisema walikuwa wakipata tabu kutokana na kauli za baadhi ya wanasiasa kudai kuwa Wazanzibari hawautaki Muungano, jambo lililobainika kuwa si kweli.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru