Thursday, 22 May 2014

SAKATA LA MTOTO ALIYEISHI NDANI YA BOKSI


Mazito  yaibuka

  •  Abainika kuathirika mifupa, Nduguye hajulikani alipo

NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
SAKATA la mtoto Nasra Mvungi (4), aliyefichwa ndani ya boksi kwa miaka mine, limechukua sura mpya baada ya mtoto huyo kufanyiwa uchunguzi na kubainika kwamba ana hitilafu kwenye mifupa.
Mtoto huyo alikuwa akiishi kwenye boksi kwa miaka minne baada ya kufichwa na wazazi wake walezi, Mariam Said na mumewe, Mtonga Omari ambao tayari wanashikiliwa na polisi.

Kutokana na hali hiyo, mtoto huyo anatarajiwa kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili yakupatiwa matibabu makubwa zaidi.
Mbali na matokea ya uchunguzi kuonyesha hali hiyo, pia imebainika kuwa kaka wa Nasra, anayeitwa Nasoro, hajulikani alipo na hivyo kuzidi kuzua hofu dhidi ya mama yao mkubwa, Mariam Said.
Akizungumza na Uhuru jana, Daktari Mshauri wa Masuala ya Watoto wa Hospitali ya mkoa wa Mrorogoro, Dk. Isaack Msaky alisema vipimo vimeonyesha kwamba mtoto huyo ana matatizo ya mifupa ya mikono na miguu.
“Tulifanya vipimo vya x-ray na kugundua kwamba mtoto huyu, ana matatizo ya mifupa, hivyo inatulazimu tumuhamishie Hospitali ya Taifa Muhimbili,”alisema Dk. Msaky.
Hata hivyo, alisema watamuhamishia Muhimbili baada ya kumpatia matibabu ya ugonjwa wa homa ya vichomi (Nimonia) unaomsumbua mtoto huyo.
Dk. Msaky alisema mbali na ugonjwa huo, pia mtoto huyo aligundulika kuwa na tatizo la utapiamlo mkali, ambao umesababisha afya yake kudhoofika.
Wakati huo huo,  mtoto mwingine, ambaye ni kaka wa Nasra, aliyefahamika kwa jina la Nasoro, hajulikani alipo hali ambayo imeendelea kuzua hofu kwa majirani.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa, Mariam aliachiwa watoto wawili baada ya mdogo wake kufariki, lakini mtoto mmoja alionekana kwa miezi kadhaa na baadaye kutoweka.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa wa Azimio anakoishi Mariam, Tatu Mgalagala, alisema kwamba Mariam aliachiwa watoto wawili, lakini mmoja haonekani.
Tatu alisema  majirani wa Mariam walisema walimuona mtoto huyo, anayekadiriwa kuwa na miaka minane, wakati wa msiba wa mama yao, lakini baada ya miezi kadhaa, mtoto hajaonekana hadi sasa.
Wakizungumza na Uhuru, majirani wa Mariam walilihusisha tukio hilo na imani za kishirikina kutokana na mazingira anayoishi mama huyo.
Walisema wakati mdogo wake anafariki, Mariam alikabidhiwa watoto wawili, Nasra na Nasoro, lakini kwa muda mrefu hawajamuona mtoto huyo wa kiume.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paul, alisema polisi bado wanafanya uchunguzi na kwamba watatoa taarifa watakapokamilisha.
Juzi polisi mkoani hapa waliwakamata Mariam na mumewe, Omari kwa tuhuma za kufanya unyama huo nyumbani kwao katika mtaa wa Azimio, kata ya Kiwanja cha Ndege.
Kamanda  Paul alisema tukio hilo lilibainika baada ya majirani kushuhudia  unyama huo, ikiwa ni pamoja na Nasra kutoonekana nje.
Alisema kutokana na kuumizwa na unyama huo, jana majirani waliamua kuizingira nyumba wanayoishi wanandoa hao, lakini polisi walipata taarifa kwa raia wema na kufika eneo la tukio.
Kamanda Paul alisema baada ya polisi kufika eneo hilo, walielezwa kinachoendelea na kuamua kufuata taratibu za kuingia ndani ya nyumba na hatimaye kumkuta Nasra akiwa kwenye boksi.
Kutokana na tukio hilo, polisi walilifikisha suala hilo katika ofisi za Ustawi wa Jamii mkoa kwa hatua za awali.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswing Ngungamtitu, alisema mtoto huyo alipokewa akiwa na hali mbaya kiafya na sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani mkoani hapa.
Alisema hali ya Nasra si nzuri na kwamba, afya yake imedhoofu kiasi cha kuonekana kama mtoto mchanga.
Ofisa huyo alisema kwa sasa Nasra yuko chini ya uangalizi wa ofisi yake huku wakisubiri hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Akizungumza na waandishi wa habari, baba mzazi wa mtoto huyo, Nassoro Rashid alisema alimkabidhi Nasra kwa Mariam na amekuwa akitoa gharama zote za matunzo ya binti yake.
Alisema kwa sasa anaye mke mwingine wa ndoa na watoto na kwamba, hakuwahi kumweleza mkewe huyo kuhusu kuwa na mtoto mwingine nje ya ndoa.
“Nimeumizwa mno na hali niliyomkuta nayo mwanangu. Nilimkabidhi kwa mama yake mkubwa na naleta matunzo kwa ajili yake kila wakati. Mara kadhaa ninapofika na kutaka kumwona, ananieleza kuwa amelala, hivyo sipati fursa ya kumuona,” alisema Rashid.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru