NA ABDALLAH MWERI
UJENZI wa kivuko kitakachotoa huduma ya usafiri kati ya Jiji la Dar es Salaam na mwambao wa Bahari ya Hindi hadi Bagamoyo, kitakamilika mwezi ujao tayari kwa kuanza kazi.
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema hayo bungeni juzi wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo na Makadirio ya Mapato na Matumizi katika mwaka wa fedha 2014-2015.
Dk. Magufuli alisema ujenzi wa kivuko hicho unaendelea nchini Bangladesh na ukamilishwaji wake utakuwa na ustawi mzuri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Bagamoyo.
Pia alisema ujenzi wa kivuko cha Kahunda/Maisome unaendelea mkoani Mwanza, sanjari na kivuko cha Msangamkuu na boti ya uokozi, itakayotoa huduma mkoani Mwanza.
Alisema ujenzi wa maegesho ya vivuko vya Msangamkuu, Muharamba, Kikumbaitale na Senga umekamilika tangu Aprili, mwaka huu.
Aliongeza kuwa utaratibu wa manunuzi kwa ajili ya kuwapata makandarasi wa ujenzi wa maegesho ya Kilambo, Ukara, Ilagara, Bugolora na Kivuko kwa usafiri wa majini kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo unaendelea.
Alisema ukarabati wa kivuko cha MV Chato umekamilika na kinaendelea kutoa huduma na ukarabati wa vivuko vya MV Kome 1 na MV Geita unaendelea mkoani Mwanza.
Dk. Magufuli alisema ukarabati wa kivuko cha MV Magogoni na MV Kilombero 1 uko katika hatua ya kumpata mkandarasi. Alisema katika mwaka wa fedha 2014-2015, mradi wa ukarabati wa vivuko vya MV Magogoni, MV Mwanza, MV Kiu na MV Pangani 11 umetengewa sh. bilioni 2.1.
Akifafanua, alisema kivuko cha MV Magogoni kimetengewa sh. milioni 660, MV Mwanza (sh. milioni 500), MV Morogoro (sh. milioni 400) na MV Pangani 11 (sh. milioni 472).
Katika hatua nyingine, Magufuli amesema ujenzi na ukarabati wa nyumba na majengo ya serikali kwa ajili ya makazi ya viongozi na watumishi, umetengewa sh. milioni 2,689.46.
Waziri Magufuli alisema kipaumbele katika ujenzi wa nyumba hizo, kimelenga kwa majaji na viongozi wengine wa serikali wenye stahiki.
Alisema katika mwaka wa fedha 2014-2015, sh. milioni 200 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa nyumba ya makazi ya mkuu wa wilaya ya Urambo.
Alisema zimetengwa sh. milioni 540 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa nyumba za majaji katika mikoa ya Shinyanga, Kagera, Mtwara, Kilimanjaro na Dar es Salaam.
Dk. Magufuli alisema sh. milioni 100 zimetengwa kuendelea na ujenzi wa uzio na kuweka mfumo wa ulinzi katika nyumba za viongozi wa serikali zilizoko Mikocheni, Kijitonyama na Msasani Peninsular.
Alisema Wizara ya Ujenzi imetenga sh. milioni 480 kwa ajili ya kufanya matengenezo na ukarabati wa nyumba za viongozi wa serikali na sh. milioni 500 kwa ununuzi wa samani.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru