Wednesday, 14 May 2014

Homa ya Dengue yaitikisa serikali



  • Mabasi ya abiria, daladala sasa kupuliziwa dawa
  • M’nyamala yafurika, wauguzi wake saba waugua
  • Sadiki atoa maagizo, serikali yatenga Mil. 500/-

NA FURAHA OMARY
SERIKALI imeziagiza Halmashauri za Manispaa za mkoa wa Dar es Salaam, kusimamia mara moja upuliziaji dawa katika maeneo yenye mkusanyiko ili kukabiliana na ugonjwa wa homa ya dengue.
Imeziagiza Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni, kutenga fedha za dharura kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.
Aidha, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imetakiwa kuandaa utaratibu wa kupulizia dawa mabasi yote yaendayo mikoani, meli na treni ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo.
Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mecki Sadiki wakati alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Taifa (TBC1), kuhusu ugonjwa huo wa dengue.
Sadiki alikuwa ameambatana na Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Grace Magembe.
“Tunasisitiza suala la usafi wa mazingira kwa kuwa bila kuboresha, tutaendelea kuugua si dengue pekee, hata magonjwa mengine, hivyo lazima tuchukue hatua za matibabu.
“Tulikuwa na kikao cha kamati ya ulinzi na usalama, hatua tuliyofikia ni kwamba manispaa zisimamie kuhakikisha maeneo yenye mikusanyiko yanapuliziwa dawa ili kukabiliana na ugonjwa huo,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema maeneo ya baa, hoteli, sokoni, vituo vya daladala pamoja na shule zote lazima yapuliziwe dawa ili kuwanusuru wananchi kung’atwa na mbu aina ya Aedes ambaye hupendelea kung’ata mchana.
“Dar es Salaam, tunabeba ugonjwa huo na tunasambazia wengine. Nimeagiza SUMATRA watengeneze ratiba kwa mabasi 600 yanayokwenda nje ya mkoa yapuliziwe dawa,” aliagiza.
Kuhusu halmashauri kutenga fedha za dharura, Sadiki alisema licha ya mkoa huo kukabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara, lakini hilo linaweza kusubiri na si mapambano na homa ya dengue.
“Manispaa ya Temeke wameshaanza kwa kununua vitendanishi na vifaa. Vituo vyote vinavyoingiza watu na kutoka, vitamwagiwa dawa ili kutosambaa. Treni zinazokwenda  bara, meli pia zitafanyiwa hivyo ili kuwanusuru wasafiri,” alisema.
Akizungumzia kuhusu homa hiyo ya dengue, Sadiki alisema ugonjwa huo ni mpya hapa nchini na kwamba ulianza kuonekana mwishoni mwa Januari, mwaka huu na tangu ulipothibitika kuwa upo Dar es Salaam, karibu watu 523 walipimwa.
Sadiki alisema kati ya watu hao, 414 walithibitika wana dengue na waliendelea kupatiwa matibabu, ambapo Kinondoni walikuwa 342, Temeke 20 na Ilala 52.
Mkuu huyo wa mkoa alisema tayari watu watatu wameshapoteza maisha, akiwemo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Temeke, Gilbert Bubelwa.
Hata hivyo, alisema wagonjwa 21 bado wapo hospitalini, ambapo sita wapo Amana, 14 wapo Temeke na mgonjwa mmoja, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Unguja Kaskazini (CCM), Bahati Ali Abeid yupo katika Hospitali ya Dk. Mvungi.
Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Grace aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha hawang’atwi na mbu.
Alisema ugonjwa huo hauna kinga wala chanjo na wataalamu wapo katika tafiti.
Dk. Grace alisema mbu huyo ana tabia ya kung’ata mchana, ikiwa ofisini, nyumbani au katika maeneo mengine, hivyo wananchi wanapaswa kufanya usafi katika maeneo yao na kutoka katika maeneo hatarishi.
Pia, aliwataka wananchi kuzibua mitaro, kufyeka nyasi, kufunika maji wanayokinga kwa kuwa mbu huyo anapenda maji masafi, waache kutupa chupa ovyo, vifuu vya nazi, matairi na mifuko ya plastiki.
Ugonjwa wa homa ya dengue unasababishwa na kirusi, ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, takriban asilimia 40 ya watu wote duniani wanaishi katika nchi zenye ugonjwa huu.
Alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani zinathibitisha kuwa takribani matukio milioni tano ya dengue yanatolewa taarifa kila mwaka.
Serikali yatenga Mil. 500/-
SERIKALI imetenga sh. milioni 500 kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa ya dengue na kuwa mpaka sasa imeshatumia sh. milioni 132.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Stephen Kebwe alisema hayo jana alipotoa taarifa ya serikali Bungeni kuhusu ugonjwa huo.
Dk. Kebwe alisema kuanzia Januari hadi sasa, watu 458 wamethibitika kuugua ugonjwa huo huku wengine watatu wakipoteza maisha.
Alisema ugonjwa huo hauambukizi kwa kumuhudumia mgonjwa au kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa.
Kwa mujibu wa Dk. Kebwe, ugonjwa huo si mpya hapa nchini kwani uligundulika kwa mara ya kwanza Juni 2010 mkoani Dar es Salaam, ambapo watu 40 walithibitika kuwa na ugonjwa huo.
Mwananyamala yafurika wagonjwa
Hali katika Hospitali ya Mwananyamala, imezidi kuwa tete baada ya watu 139, wakiwemo wauguzi saba, kukutwa na virusi vya ugonjwa huo kati ya 333 waliofanyiwa vipimo.
Daktari Kiongozi wa Idara ya Wagonjwa wa Nje, Dk. Mrisho Lupinda, alisema watu wengine 194 wamebainika kuwa na dalili za ugonjwa huo ambao umeshaua watu wawili katika hospitali hiyo.
Pia, alisema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mlundikano wa wagonjwa waliofika kwenda kupima ili kuchunguza  afya zao, hali inayosababisha wauguzi kuzidiwa na kuanza kuchuja yupi apimmwe na yupi asipimwe kutokana na dalili watakazoziona.
Aliwataka wananchi kutumia dawa za kupaka za kuzuia mbu na kuvaa nguo ndefu, kupuliza dawa za mbu kwenye makazi yao ili kudhibiti ugonjwa wa dengue.
Dk. Lupinda alisema mbu hao walikuwepo tangu miaka 300 iliyopita, lakini hapa nchini hakukuwa na virusi, na sasa hali hiyo imejitokeza kutokana na mwingiliano wa kibiashara baina ya nchi moja na nyingine na kwamba ugonjwa huo umeshamiri katika eneo la mashariki ya mbali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru