Friday, 16 May 2014

Mrema: Askari Polisi wapewe asilimia 10 mali wanayokamata


NA WAANDISHI WETU, DODOMA
BAADHI ya wabunge wamependekeza askari polisi kupewa asilimia 10 ya thamani ya mali wanayokamata ili iwe kichocheo cha kufanya kazi kwa bidii na kuacha kuomba na kupokea rushwa.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Augustine Mrema (Vunjo ñ TLP) alisifu utendaji wa jeshi la polisi na kushauri kuwa wawe wanapewa motisha kwa lengo la kuwapa morari ya kufanya kazi zaidi ya ilivyo sasa.


Mrema alisema kwa kufanya hiyo kutasaidia kupungua kwa vitendo vya uhalifu nchini kwani hali hiyo itawaongezea askari moyo wa kufanya kazi.
Mbunge huyo alishauri askari kupewa hata asilimia 10 ya thamani ya mali anayokamata kama kichocheo kwake kufanya kazi kwa bidii.
Pia, alishauri askari kuongezewa posho kutoka sh. 5,000 ya sasa mpaka 7,500 kwa sababu fedha hiyo ya awali, haiwezi kuwafanya askari kujikimu katika mahitaji ya kila siku.
Mbunge mwingine, Catherine Magige (Viti Maalumu ñ CCM) aliipongeza wizara kwa kazi nzuri huku akisifu utendaji kazi wa Jeshi la Polisi licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa.
Kazi wanayoifanya askari polisi ni kubwa sana,  ni vyema serikali ikaangalia namna ya kuboresha maslahi kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu,î alisema Catherine.
Pia, Catherine alimmwagia sifa Kamishna wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile,  kwa kuweka mambo sawa katika idara hiyo.
Kwa kweli, Rais (Jakaya) Kikwete amefanya uteuzi sahihi kabisa kwa AmbokileÖ hivi sasa pamoja na mambo mengine, upatikanaji wa pasi za kusafiria umekuwa rahisi sana,î aliongeza. 
Kwa upande wake, Hasnai Murji (Mtwara Mjini - CCM) alishauri uhusiano kati ya wananchi na jeshi la polisi mkoa wa Mtwara kudumishwa ili kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo.
Alisema hivi sasa mambo yako shwari baada ya hali ya amani kupotea katika kipindi cha hivi karibuni.
ìWananchi wa Mtwara wameelewa. Kilichokuwa kiikihitajika kwao ni elimu. Tumewapa na sasa Mtwara kuna amani na utulivu. Tunaamini sasa wawekezaji wengi watakimbilia mkoani kwetu kwa ajili ya uwekezaji,î alisema.
Aliasa matumizi ya kutumia nguvu yanayofanywa na askari polisi dhidi ya waendesha bodaboda kwani yanasababisha kuongezeka kwa chuki kwa vijana hao.
Faida Bakary aliitaka serikali kuongeza maslahi kwa askari polisi kwani wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu.
Wizara ya Mambo ya Ndani imeomba kiasi cha sh. 881, 740, 291, 800 kwa ajili ya mwaka mpya wa fedha wa 2014/2015.
Katika hatua nyingine, serikali imesema  katika mwaka wa fedha 2013/2014, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imesajili watu 3, 300, 119 katika visiwa vya Unguja na Pemba na jijini Dar es Salaam.
Akiwasilisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,  Waziri Mathias Chikawe, alisema wakazi 2, 449, 822 jijini Dar es Salaam na watu 560, 297 kwa Unguja na Pemba wamesajiliwa.
Chikawe alisema NIDA inaendelea na jukumu lake la msingi la kujenga mfumo wa usajili na utambuzi wa watu nchini ambayo moja ya matokeo yake ni utengenezaji wa vitambulisho vya taifa.
Alisema mfumo huo utaiwezesha serikali katika ukusanyaji wa mapato na kuwawezesha wananchi wengi kukopesheka kwa maana kwamba watakuwa wakitambulika na kusaidia udhibiti wa usalama wa nchi.
Waziri alisema, katika mwaka wa fedha uliopita, serikali iliongeza vifaa vya usajili 280 ëMobile Enrolment Unití (MEU), ilikamilisha ujenzi wsa kituo cha muda cha kuingiza taarifa na kutunza kumbukumbu.
Alisema, serikali imeanza mchakato wa awali wa kituo kikuu cha utunzaji wa kumbukumbu na kile cha uokozi wakati wa majanga na vituo 13 vya usajili wa wilaya ambapo ujenzi huo utafanywa kwa fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Korea.
Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ilipendekezwa NIDA kuongezewa fedha kwani mamlaka hiyo ilitengewa sh. bilioni 151 kwa ajili ya kazi yao ya usajili na utambuzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo inayoongzwa na Anna Abdallah, mpaka kufikia Machi mwaka huu, fedha zilizotolewa kwa NIDA ni sh. bilioni 34 tu.
Kamati hiyo imeshauri fedha zilizobaki zitolewe mapema kwani upungufu wa fedha utasababisha utoaji wa vitambulisho kutokamilika kwa wakati. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru