NA THEODOS MGOMBA,DODOMA
AJALI za barabarani zimeongezeka kwa asilimia 3.7 kwa mwaka jana ukilinganisha na zilizotokea mwaka 2012.
Kauli hiyo ilitolewa juzi jioni na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake.
Pia alisema kumekuwa na ongezeko la idadi ya majeruhi na vifo vinavyotokana na ajali hizo.
Chikawe alisema takwimu zinaonyesha katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2012, ajali za barabarani 23,604 zilitokea katika maeneo mbalimbali na watu 4,062 walipoteza maisha na wengine 20,037 walijeruhiwa.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2013 ajali zilizotokea ni 24,480 ambazo zilisababisha vifo vya watu 4,091 na wengine 21,536 kujeruhiwa.
Chikawe alisema sababu kubwa ya ongezeko la ajali za barabarani ni mwendo kasi, ulevi, uzembe wa madereva, ubovu wa vyombo vya usafiri na kubeba abiria na mizigo kuliko vyombo husika .
Alisema vifo vimeongezeka kwa asilimia 3.4 na majeruhi wameongezeka kwa asilimia 7.5 katika kipindi cha mwaka 2012/2013.
Waziri Chikawe alisema Jeshi la Polisi katika mwaka huu wa fedha litaimarisha doria, misako na operesheni maalumu ili kupunguza matishio ya uhalifu, makosa ya jinai na ajali za barabarani.
Pia, alisema Jeshi litaendelea kujiweka tayari kudumisha amani na utulivu katika kipindi cha kwenda kwenye upigaji wa kura za maoni ya kupata katiba mpya , uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Aidha Chikawe alisema katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2013 jumla ya makosa makubwa ya jinai 560,451 yaliripotiwa katika vituo vyote vya polisi nchini ikilinganishwa na makosa 566,702 yaliyoripotiwa mwaka 2012.
Alisema idadi ya makosa hayon yaliyoripotiwa yamepungua kwa asilimia 1.1 upungufu ambao unatokana na upatikanaji wa taarifa za uharifu mapema na utekelezaji wa Polisi Jamii unahusisha wananchi.
Chikawe alisema makosa makubwa yaliyoripotiwa yapo katika makundi makubwa matatu ambayo ni makosa dhidi ya binadamu, makosa ya kuwania mali na makosa dhidi ya maadili ya jamii.
Waziri huyo alisema makosa wa kuwania mali yamepungua kutoka 46,773 mwaka 2012 hadi 45,470 mwaka 2013.
Friday, 16 May 2014
Ajali za barabarani bado tishio - Chikawe
08:36
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru