Thursday, 8 May 2014

Wizi wa mafuta magari ya serikali kudhibitiwa


NA JESSICA KILEO
SERIKALI imeanza kutekeleza mradi wa kufunga mfumo wa kielektoniki wa kudhibiti matumizi ya mafuta kwa vyombo vya moto vya umma (FMS), ambao utafungwa katika magari na mitambo ya taasisi za umma.
Mitambo hiyo itasaidia kudhibiti matumizi ya fedha za umma yanayofanywa na baadhi ya watumishi kupitia ununuzi wa vifaa mbalimbali na mafuta.
Pia, mfumo huo unatarajiwa kuanza majaribio katika kituo cha mafuta cha Kurasini mwishoni mwa Julai, mwaka huu, ambapo mtaalamu wa kampuni ya Net-soft Consult (T) ameanza kazi ya kusimika mfumo huo katika kituo hicho.
Mkurugenzi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), Yoswam Nyongera, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kuhusu mfumo huo mpya.
Nyongera, alisema mradi huo utatekelezwa na GPSA ambao utashirikisha wizara na taasisi zote za umma, ambazo kwa mujibu wa sheria ya ununuzi wa umma namba saba ya mwaka 2011 sura ya 410 kifungu cha 56, zinatumia huduma hiyo kutoka kwa wakala.
Alisema mfumo huo ambao unatumika kimataifa na hasa mataifa yaliyoendelea, utakuwa wa kwanza kutumika katika taasisi za umma Afrika.
Pia, alisema mfumo huo wa kielektroniki wa kudhibiti ujazaji wa mafuta katika magari na mitambo ya serikali ni moja kati ya malengo ya wakala ya kuhakikisha matumizi mabaya ya fedha hayatokei.
“Mfumo huu utasaidia kudhibiti udanganyifu katika utoaji wa mafuta kwa magari ya serikali na kuhakikisha kuwa hakuna upotevu wa mafuta utakaojitokeza,”  alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Himili Biashara wa GPSA, Maliki Aram, alisema uwezo wa mfumo huo ni pamoja na kutambua gari na mitambo kwa ajili ya kupatiwa mafuta, kutunza kumbukumbu za malipo ya mafuta na hivyo kutoa mafuta kwa kadiri ya fedha iliyolipiwa. 
Alisema mfumo huo utatambua kiwango na ubora wa mafuta yaliyomo kwenye mantenki ya kutunza mafuta kila wakati, ina uwezo wa kutuma ujumbe mfupi kwa njia ya barua pepe kwa kiasi cha mafuta kilichochukuliwa kwa taasisi husika mara baada ya gari au mtambo kupatiwa mafuta.
Aram, alisema mfumo huo utasaidia kutuma taarifa za matumizi ya mafuta kwa kila gari au mtambo huo utaonekana kwa taasisi itakayounganishwa.
Alisema baada ya kukamilika kwa mfumo huo katika kituo cha Kurasini kwa mwaka huu wa fedha, wanatarajia mwaka ujao wa fedha kuupeleka na kuufunga katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Mbeya na Mwanza.
Naye, Mkurugenzi wa Uendeshaji GPSA, Naftali Sigwejo, alisema katika hatua ya awali, mfumo huo utaweza kuonekana katika tovuti ya wakala na kuunganishwa katika mikoa yote, ambapo miundombinu itakuwepo Dar es Salaam na kuunganishwa mikoa mingine kwa njia ya mtandao.
Sigwejo, alisema hatua hizo zitahusisha kufungwa kwa kifaa maalumu ‘Identification TAG’ katika mlango wa tanki la gari au mtambo, ambapo kitakuwa na uwezo wa kutambua gari au mtambo husika kabla ya kupatiwa huduma ya mafuta.
Pia, alisema kuna kifaa kingine kitaunganishwa ambacho ni sense, kitakachofungwa kwenye pampu ya mafuta kitachotambua gari au mtambo husika, ambapo hakutakuwa na haja ya mawasiliano kati ya dereva na muhudumu wa pampu tena.
Alisema mfumo huo kwa ujumla utasaidia kuondoa udanganyifu wa matumizi ya mafuta kwenye magari na mitambo kwa taasisi za umma.
“Chombo cha umma kitakachodhibitika ndicho pekee kitaweza kupatiwa mafuta na taarifa ya matumizi yake zitapatikana kwa wakati kupitia mtandao, hivyo uamuzi sahihi kufanyika juu ya matumizi ya mafuta kwa chombo husika,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru