Thursday, 15 May 2014

Makandarasi 752 wafutwa kazi


NA EVA-SWEET MUSIBA, MWANZA
BODI ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imefuta usajili wa makandarasi 752 kutokana na makosa mbalimbali, yakiwemo ya kutofanya kazi kwa kiwango na uvunjaji wa sheria.
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Mhandisi Boniface Muhegi, alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza jana, Mhandisi Evarist Ndikilo, katika Mkutano wa 16 wa mashauriano wa usajili wa makandarasi ya mwaka huu.
Muhegi, alisema katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu Tanzania (BOT) Jijini Mwanza, alisema makandarasi hao walifutwa kutokana na makosa mbalimbali.
Alisema makandarasi wanane wamefutwa kutokana na kukiuka sheria ya Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), ambao walipewa malipo ya awali na wakakimbia eneo la kazi bila kufanya kazi kwa mujibu wa mkataba waliokubaliana.
Ndikilo, akifungua mkutano huo, aliwataka makandarasi hao kutafuta fursa za kazi kwa kutumia njia ya ubia itayakayowasaidia  kujenga uwezo na kufanya kazi kwa ubora.
“Kuna makandarasi 13 walijiunga kwa pamoja katika ujenzi wa Daraja la Mbutu Wilaya ya Igunga, walifanya kazi nzuri, nawaomba muige mfano wao,” alisema Ndikilo.
Aliwataka waajiri kuwapa kipaumbele makandarasi waliojiunga katika kutafuta kazi kwa ubia.
Alisema CRB nayo ihakikishe inawasaidia makandarasi kupata usajili ili waweze kupata fursa hizo za kazi.
Hata hivyo, aliwaonya makandarasi kutoparamia kazi wasizoziweza na kusababisha hasara kwa mashirika yanayowapatia kazi. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru