Tuesday, 20 May 2014

Hakuna adhabu ya kifo kwa wezi na wahujumu -Migilo


WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, amesema serikali haina mpango wa kutunga sheria inayotoa adhabu ya kifo kwa wezi na wahujumu uchumi.
Amesema adhabu ya kifo ama kunyongwa hadi kufa hutolewa kwa watuhumiwa wa makosa ya uhaini, kuua ama kuua bila kukusudia.
Asha-Rose alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Moses Machali (Kasulu Mjini-NCCR-Mageuzi), aliyetaka kujua  mpango wa serikali katika kutunga sheria kali dhidi ya wezi na wahujumu uchumi nchini, ikiwemo ya kunyongwa hadi kufa.
ìSerikali kwa sasa haina mpango wa kutunga sheria inayotoa adhabu ya kifo kwa wezi na wahujumu uchumi kwani inaamini sheria zilizopo ni kali vya kutosha na zitaendelea kufanyiwa marekebisho kwa kadri inavyohitajika,îalisema.
Alisema endapo mtu atatiwa hatiani kwa kosa la uhujumu uchumi, anaweza kuhukumiwa kifungo kisichozidi miaka 15 jela, kulipa faini au vyote kwa pamoja.
ìMakosa ya uhujumu uchumi yanadhibitiwa na sheria ya uhujumu uchumi, sura ya 200 ambapo yapo ya aina nyingi na baadhi yake ni kusababisha hasara kwa mamlaka, na makosa yaliyo chini ya sheria ya wanyama pori,î alisema.
Alisema makosa ya wizi yanadhibitiwa na sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16 na kwamba adhabu zake zinatofautiana, zikianzia faini, kifungo cha muda mfupi au mrefu kinachoweza kufikia miaka 15 jela kwa kutegemea uzito na mazingira ya kosa.
Aliyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ni wizi wa kawaida kwa mtu kuchukua kitu cha mtu mwingine bila ridhaa yake, wizi wa kuaminiwa au wizi unaofanywa na mtu aliye katika utumishi wa umma.
Hata hivyo, Asha-Rose alisema serikali inaamini kuwa sheria zilizopo ni kali vya kutosha na zitaendelea kufanyiwa marekebisho kadri itakavyohitajika.
Alisema pamoja na ukweli huo, nia ya kutoa adhabu ni kuzuia na kudhoofisha uhalifu, kuwarekebisha wahalifu na kurejesha mali iliyoibwa.
Aliwataka wananchi kujenga utaratibu wa kutoa taarifa ya kuwepo kwa matukio ya kiharifu na uhujumu uchumi kwenye maeneo yao badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Alisema kwa sasa wananchi wanashirikishwa katika mfumo wa polisi jamii na ulinzi shirikishi ili kuendelea kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru