Thursday, 22 May 2014

Bil. 220/- kutumika kujenga minara ya mawasiliano


ABDALLAH MWERI, DODOMA
SERIKALI inatarajia kutumia sh. bilioni 220 kwa ajili ya ujenzi wa mawasiliano katika mikoa yote ya Tanzania Bara kabla ya mwaka 2015.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
January, alikuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge Selemani Zedi (Bukene-CCM), aliyetaka kujua ni lini serikali itajenga minara ya kutosha katika maeneo ya vijijini nchini.
Alisema wizara yake inatarajia kupata sh. bilioni 154 ilizoomba kutoka serikali ya India, ambazo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano nchini.
Alisema  dhamira ya serikali ni kujenga minara mingi ili kuwapa fursa wananchi kupata mawasiliano kwa uhakika.
January alisema pia kuwa, wizara yake ina mpango mkakati wa kujenga minara ya kutosha ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani, ikiwemo mikoa ya Ruvuma na Kagera.
“Wizara imedhamiria kujenga minara mingi maeneo yote ya Tanzania yaliyokosa mawasiliano. Binafsi nilikwenda India kuomba fedha na tunatarajia kupata sh. bilioni 154, ambazo zitatumika kwa ujenzi wa minara,” alisema January.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru