Sunday, 25 May 2014

Kinana: Utekelezaji Ilani umefanikiwa

NA Mohammed Mussa, Iramba.

  • Nape asema ‘Katiba ya Watanzania bila UKAWA inawezekana’

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amewahakikishia wanachama na wananchi kuwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2010-2015, chini ya Rais Jakaya Kikwete, unakwenda vizuri.

Amesema katika ziara zake za

kukagua utekelezaji wa ilani kwenye mikoa mbalimbali nchini, umefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba kazi iliyobakia ni ndogo.

Kinana alisema wanachama na wananchi wana kila sababu ya kujivunia kutokana na Chama, kutekeleza kwa vitendo ahadi ilizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Alisema kwa kushirikiana na viongozi wenzake watahakikisha CCM, inazidi kujiimarisha ili iweze kuwatumikia Watanzania.

Kinana alisema hayo Wilaya ya Iramba Mashariki mkoani Singida, baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya wilaya hiyo.

Alisema lengo la ziara zake ni kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, uhai wa Chama na maandalizi ya uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa.

Kinana alisema Chama chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, kimefanya mambo mengi katika jamii na kwamba asilimia kubwa ya ahadi zake imezitekeleza.
 

Hakuna anayekamilisha kila kitu, lakini mambo mengi tuliyoahidi tumeyatekeleza na wananchi ni mashahidi,î alisema na kuwa ni lazima Chama, kizidi kujiimarisha na kujengwa upya ili kiweze kutatua matatizo ya wananchi," alisema.

Kinana alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, Chama kitaibuka na ushindi mkubwa.

Alisema CCM, ndio yenye jukumu la kuzunguka nchini na kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana baada ya uchaguzi hadi sasa kwa kuwa wapinzani wanataka viongozi wa Chama, wasizunguke ili wapate la kusema.

Alisema miradi mbalimbali imetekelezwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, umeme, shule, maabara, afya na mawasiliano.

Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Kinana alisema baadhi ya viongozi wameugeuza mchakato huo kuwa mazingaombwe.

Alisema katiba wanayoitaka wapinzani ni ya kuwaweka madarakani na wala si ya kuleta maendeleo katika jamii.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) Mwigulu Nchemba, ametoboa siri ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kutoka ndani ya Bunge, kuwa wanafanya majaribio kwani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,wengi hawatarudi bungeni.

Amesema baadhi ya wajumbe hao ambao pia ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watakosa ubunge, hivyo wanafanya mazoezi ya kurejea uraiani.

Mwigulu alisema wabunge wengi ambao wamejiunga na UKAWA baada ya uchaguzi mkuu hawatakanyaga tena ndani ya Bunge na wataishia mapokezi au sehemu za kufikia wageni.

Kauli hiyo, aliitoa wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Tarafa ya Shelui wilaya ya Iramba Mashariki mkoani Singida.

Mwigulu ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema UKAWA hawana sababu ya msingi ya kutoka bungeni.

Alisema baada ya UKAWA kushindwa kwa hoja, walifanya kila hila kutafuta sababu za kususia Bunge Maalumu la Katiba na kwamba sababu zao hazina msingi wowote.

Mwigulu alisema Bunge Maalumu la Katiba litakapoendelea tena Agosti, mwaka huu, watashauri posho zilipwe kila baada ya wiki moja.

Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema wasiotaka katiba mpya, ipo ya zamani ambayo itatumika.

Alisema vyama vya siasa vinaigiza ili vipate kula na kwamba katika kuigiza kwao, vinataka watu wote wawaamini.

Nape alisema CCM, ndio Chama pekee ambacho kikipanga mambo yake, kinamaanisha na kutekeleza.

Alisema CCM inazidi kuimarika na kukubalika katika jamii kwa sababu ndiyo kinacholeta maendeleo nchini na kuwa: Katiba ya Watanzania bila ya UKAWA inawezekani.”

Alisema kama UKAWA hawautaki mchakato wa katiba, waachwe waende barabarani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru