Thursday, 22 May 2014

Kebwe: Maambukizi ya malaria yamepungua


WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, imesema maambukizi ya ugonjwa wa malaria yamepungua kwa asilimia 47 kati ya mwaka 2008 na 2013.
Akijibu swali bungeni jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Steven Kebwe alisema mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria nchini yamechangia kupungua kwa vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.
Alisema vifo hivyo vimepungua kutoka 148 kwa kila vizazi hai 1,000 waliozaliwa mwaka 1995-1999 hadi kufikia vifo 54 mwaka 2013.
Dk. Kebwe alikuwa akijibu swali la  Moza Saidi (Viti Maalumu-CUF), aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na serikali katika kupambana na ugonjwa huo.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za tafiti za viashiria vya ugonjwa wa malaria ngazi ya jamii, kiwango cha uwepo wa malaria mwaka 2008 kilikuwa asilimia 18 na mwaka 2012 kilishuka hadi asilimia 10.
“Wizara inahimiza juu ya matumizi sahihi ya dawa za kutibu malaria ili kuzuia kujitokeza kwa malaria sugu, matumizi ya vyandarua vyenye viatilifu, kutumia nyenzo za kinga kama usafi wa mazingira, kudhibiti mazalia ya mbu na upulizaji wa dawa majumbani,” alisema.
Alisema serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kupambana na ugonjwa wa malaria nchini na miongoni mwa juhudi hizo ni kuwepo kwa dawa za kutibu malaria ya kawaida na kali katika vituo vya afya.
Alizitaja hatua zingine kuwa ni kugawa vyandarua vyenye uatilifu, kutoa dawa za kukinga malaria kwa mama wajawazito na kuelimisha jamii.
Aidha, alisema wizara kwa kushirikiana na serikali ya Cuba, imejenga kiwanda cha mradi wa dawa za kuua viluwiluwi kilichoko Kibaha, Pwani.
Wakati huo huo, serikali imesema dawa ya mseto imethibitika kuwa na uwezo wa kutibu ugonjwa wa malaria ya kawaida wakati kwinini inatibu malaria sugu baada ya kupimwa na wataalamu katika maabara.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru