Na Latifa Ganzel, Morogoro
MTOTO Nasra Mvungi (4), aliyekuwa akiishi ndani ya boksi kwa miaka minne, amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro, Dk. Rita Lyamuya, alisema jana kuwa, Nasra amehamishiwa Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa vipimo zaidi na kupatiwa matibabu.
Dk. Rita alisema hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri, lakini amehamishiwa Muhimbili ili kupata huduma za mifupa, ambazo hazipo katika hospitali ya mkoa wa Morogoro.
“Ilikuwa apelekwe Muhimbili Mei 27, lakini tuliamua kumpeleka mapema baada ya kuona hali yake inaendelea vizuri na pia baada ya kupata usafiri,” alisema.
Alisema wameshawasiliana na mama anayemlea mtoto huyo, ambaye aliwajulisha kwamba walifika Dar es Salaam salama na kwanza ameshaanza kupatiwa matibabu.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa mkoa wa Morogoro, Oswing Ngungamtitu, alisema licha ya mtoto huyo kuhamishiwa Muhimbili, bado ataendelea kuwa chini ya usimamizi wa ofisi yake.
Alisema kwa sasa, mtoto huyo amepatiwa mama mlezi, Josephin Joel, ambaye atakuwa akiishi naye kwa muda, akiwa hospitali kwa ajili ya kumpatia huduma zote muhimu.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru