NA WILLIAM SHECHAMBO
MKE wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria, amesikitishwa na jinsi baadhi ya watu wanavyomkosoa mwasisi huyo kwa kuwa enzi za uhai wake alifanya kazi kwa bidii katika kulitumikia taifa kiasi cha wakati mwingine kuisahau familia kwa muda.
Pia, amesema mambo yanayoendelea nchini kwa sasa ni matokeo ya tamaa na kupungua kwa upendo miongoni mwa jamii jambo linalohatarisha usalama na amani ya nchi.
Mama Maria alisema ukosoaji wa viongozi waasisi ni tatizo la dunia nzima ambalo limekuwa jinamizi kama ilivyotokea kwenye nchini mbalimbali ikiwemo Misri na Libya, hivyo ili Tanzania iweze kuepukana nalo ni wajibu wa kila mtu kuombea taifa kwa kufikiria tulikotoka na tulipo.
Alisema ni wazi kuwa Mwalimu Nyerere alifanya kazi kwa bidii hata kuisahau familia muda mwingine, kwa sababu aliwapenda Watanzania pasipo ubaguzi wowote na kama alikosea mahali ilitokea kwa kuwa na yeye ni binadamu. Hivyo haipaswi watu kumsema tofauti kama wanavyomsema sasa.
Aliyasema hayo jana nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam alipozungumza na baadhi ya wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na wenzao walio nje ya umoja huo ambao ni wakereketwa wa amani nchini, waliokwenda kumfariji.
Vijana hao walifanya hivyo ili ya kumfariji na familia yake kutokana na baadhi ya wanasiasa kutumia nafasi zao vibaya kuwakejeli waasisi wa taifa tofauti na uhalisia.
Akisoma ujumbe wa vijana hao mbele ya Mama Maria, kiongozi wa msafara huo ambaye ni Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Pwani, Mohammed Nyundo, alisema wanatambua kuwa wachache wanaowakejeli waasisi wa Tanzania wanaendeshwa na mataifa ya Magharibi na Ulaya.
Alisema kwa pamoja kama vijana wazalendo nchini wanalaani vitendo hivyo ambavyo vinataka kuipeleka nchi shimoni.
Pia, alisema wamefedheheshwa kuona Bunge tukufu linatumika kama chombo cha kuwatusi waasisi akiwemo Mwalimu Nyerere na kuitaka serikali iondoe kinga kwa watu wanaofanya vitendo hivyo ndani ya Bunge bila kuchelewa.
Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe waliokuwa kwenye msafara huo ambaye ni Mwenyekiti wa Vijana Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Japhari Mghamba, alisema anaungana na vijana wenzake kukemea tabia za wachache kuwakebehi waasisi wa taifa hili, hatua ambayo inayotakiwa kuchukuliwa na kila mwananchi mzalendo wa taifa hili bila kuchelewa.
Katika ziara hiyo, vijana hao walipanda miti kwenye eneo la nyumba ya Mama Nyerere kama alama ya upendo kwa familia ya Hayati Mwalimu Nyerere na ukumbusho wa tukio hilo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru