Sunday, 25 May 2014

Rais Zuma aapishwa

Na Joseph Damas, Pretoria

RAIS Jacob Zuma wa Afrika Kusini, amekula kiapo kuliongoza taifa hilo kwa muhula wa pili wa miaka mitano huku akiahidi kuboresha utendaji wa serikali.

Pia, ameahidi kuendelea kupambana na vitendo vya rushwa miongoni mwa baadhi ya watumishi wa umma.

Hafla ya kuapishwa kwa Rais Zuma ilifanyika jana kwenye Jengo la Union mjini hapa, imeandika historia nyingine kwa wananchi wa Afrika Kusini, ambapo ilikwenda sambamba na Maadhimisho ya miaka 20 ya Demokrasia na Uhuru tangu kuondolewa kwa utawala wa kibaguzi.

Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa wageni 400 wakiwemo marais na wakuu wa serikali kutoka mataifa mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo.

“Tutaendelea kuimarisha utendaji wa serikali na kupambana na rushwa katika utumishi wa umma ili kuendelea kuwahudumia wananchi wetu kwa kuwapa huduma zote muhimu. Tumefanya mambo mengi ya maendeleo katika kipindi kifupi, lakini bado tunapaswa kuendelea kuboresha zaidi,” alisema Zuma.

Huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye viwanja vya Union, Rais Zuma aliwapongeza wananchi kwa kumchagua kuongoza tena taifa hilo huku akiwahakikishia kuwa amelipokea jukumu hilo.

Amesema ushindi wake ni ishara kuwa wananchi wa Afrika Kusini wameendelea kukiamini Chama cha African National Congress (ANC).

Hata hivyo, alisema jukumu la kuongoza taifa hilo ni la wananchi wote bila kujali rangi na kwamba, umoja na mshikamano unahitajika ili kuendelea kulivusha taifa hilo.

Alisema jukumu kubwa lililombele yake kwa sasa ni kuendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kutengeneza nafasi za kutosha za ajira hususan kwa vijana.

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni Rais Robert Mugabe (Zimbabwe), Salva Kiir (Sudan Kusini), Makamu wa Rais wa Angola, Manuel Vicent, Goodluck Jonathan (Nigeria), Ian Khama (Botswana).

MAMBO YALIVYOKUWA


Wananchi wa Afrika Kusini walianza kuwasili viwanja vya Union saa 10 alfajiri, ambapo ulinzi katika eneo hilo uliimarishwa maradufu.

Walioruhusiwa kufika kwenye jengo la Union ni viongozi wa serikali, wakuu wa nchi na wageni wengine waliokaribia 4000.

Idadi kubwa ya wananchi ilikuwa imefurika kwenye viwanja hivyo mbali kidogo na jengo hilo na kila kilichokuwa kikiendelea waliona kupitia luninga kubwa zilizowekwa uwanja hapo.

Wasanii na wanamuziki maarufu karibu wote wa Afrika Kusini walikuwa wakitoa burudani kwa wananchi, ambapo baada ya wageni wote kufika na kuketi katika nafasi zao, Rais Zuma aliwasili tayari kwa kuapishwa.

Rais Zuma aliwasili eneo la tukio saa 11:00 akiwa ameongozana na mkewe Mantuli, ambapo umati ulilipuka kwa furaha huku nyimbo za kumsifu za kila aina zikisikika kutoka kila upande.

Jaji Mkuu wa Afrika Kusini, Mogoeng Mogoeng alimwapisha rasmi Zuma kuwa kiongozi wa taifa hilo na baadaye mizinga pamoja na ndege za kivita zilipamba anga ikiwa ni kutoa salamu za utii kwa kiongozi huyo.

Mara baada ya kuapa na kuhutubia taifa huku akitumia muda mfupi katika hotuba yake, Zuma alishuka chini na kwenda kupanda jukwaani mahali ambako wananchi walikuwa wamekusanyika.

Kwa mara nyingine tena, Zuma aliwaeleza wananchi dhamira yake ya kuhakikisha maendeleo zaidi yanapatikana ikiwa ni pamoja na kuimarisha utendaji.

Rais Zuma anatarajiwa kutangaza Baraza la Mawaziri leo, ambapo ameahidi ni wachapakazi  na waadilifu ndio watapewa nafasi ya kuungana naye.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru