NA AMINA KINGAZI, TANGA
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda, amekemea tabia ya migogoro inayojitokeza baina ya mameya na wenyeviti wa halmashauri, kuwa inaendekeza maslahi binafsi badala ya maendeleo ya wananchi.
Alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa anfungua Mkutano Mkuu wa 30 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwenye ukumbi wa Naivera Complex jijini Tanga. Mkutano huo wa siku nne, ulianza jana.
“Kitendo kilichotokea Manispaa ya Bukoba hakijanipendeza hata kidogo, kwa sababu kitasababisha Manispaa hiyo ishindwe kutumia sh. Biliomi 17 ambazo zilitengwa kwa ajili ya kazi za maendeleo za wananchi wa mji wa Bukoba.
“Tulimuomba Meya ajiuzulu ili kuleta amani. Hii ni kwa sababu vikao vilikuwa havifanyiki kutokana na malumbano yaliyokuwepo. Yeye mwenyewe akatamka rasmi kuwa anajiuzulu, wakaleta barua rasmi nami nikawajibu kuwashukuru... baadaye madiwani wakaenda mahakamani na kufungua kesi kupinga vikao visifanyike.
“Kuna sh. Bilioni 17 zimetengwa kwa ajili ya kazi za maendeleo na kuboresha Manispaa ya Bukoba, lakini hizi zitarudishwa zilikotoka kwa sababu ya kujali maslahi binafsi. Wanaoteseka ni wananchi wa Bukoba wasio na kosa lolote,” alisema Pinda.
Hata hivyo, aliwasihi mameya na wenyeviti wa Halmashauri waache ubinafsi na waweke mbele maslahi ya wananchi. Alisema inapotokea mtu mmoja kajiuzulu kwa ajili ya watu wengi, ni baraka.
Waziri Mkuu Pinda, alitumia fursa hiyo kuwataka mameya na wenyeviti hao kulishughulikia tatizo la uhaba wa madawati na kuhakikisha linakwisha, kwakuwa nyenzo wanazo kupitia Halmashauri wanazoziongoza.
“Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Tanzania ina mahitaji ya madawati 3,302,678, wakati madawati yaliyopo ni 1,837,783. Kwa hiyo, tuna upungufu wa madawati 1,464,895 katika shule zetu za msingi,” alisema Waziri Mkuu.
Alihoji iweje Mameya wakubali kuona wanafunzi wakikaa chini wakati mbao wanazikamata kila uchao kasha wanazipiga mnada.
Aliwataka wazitumie kutengeneza madawati ili kupunguza kero hiyo ambayo alisema imedumu kwa muda mrefu.
Pinda, alisema amevutiwa na waandaaji wa kipindi cha ‘Maisha Plus’ ambao wameweza kutengeneza madawati 30 katika kipindi kifupi.
“Hapa nimebaini tatizo siyo fedha, bali ni dhamira. Kama ‘Maisha Plus’ wameweza, kwa nini sisi tunashindwa,” alihoji Pinda.
Aliwataka viongozi hao waweke lengo la kuhimiza makazi bora kwa wananchi.
“ALAT inatimiza miaka 30, wekeni azimio la kuhakikisha mnaboresha makazi ya wananchi mnaowaongoza.
“Wekeni utaratibu wa kujenga nyumba 20 za kisasa kila mwaka katika kila kijiji, hili linawezekana mkiamua,” alisema Pinda.
Wednesday, 14 May 2014
Migogoro ya Halmashauri yamkera Pinda
08:32
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru