NA MUSSA YUSUPH
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limeendelea kupambana na kundi la wahalifu, maarufu kwa jina la 'mbwa mwitu', ambapo idadi ya waliokamatwa imefikia 165 baada ya wengine kumi kukamatwa jana.
Pia limesema litaweka hadharani majina ya watuhumiwa wote waliokamatwa baada ya kukamilisha operesheni hiyo ya kuwasaka mbwa mwitu.
Watu hao walikamatwa juzi jioni katika maeneo ya Kigogo, ikiwa ni mwendelezo wa harakati za jeshi hilo katika kulisambaratisha kundi hilo.
Akizungumza na Uhuru jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Suleimani Kova alisema vijana hao ni miongoni mwa watuhumiwa wanaojihusisha na vitendo vya uporaji na ukabaji chini ya kundi hilo.
Kamishna Kova alisema baada ya mahojiano kukamilika, majina yao yatawekwa hadharani pamoja na kufikishwa katika vyombo vya sheria kujibu makosa yao.
Wakati huo huo, wakazi wa maeneo ya Kigogo wamelipongeza jeshi hilo kwa kulidhibiti kundi hilo kwenye makazi yao.
Walisema sasa wanaweza kufanya shughuli zao bila bugudha kutoka kwa kundi hilo na kutaka kuongezwa kwa msako dhidi yao.
"Kukamatwa kwa Athumani Saidi, ambaye ni kiongozi wa kundi hilo kwenye maeneo yetu ni jambo zuri kwani alikuwa akitusumbua kila kukicha" alisema Shahibu Mkumbo mkazi wa eneo hilo.
Pia aliliomba jeshi hilo kufanya doria za mara kwa mara katika uwanja ujulikanao kama 'Chaukucha', ulioko maeneo hayo, hasa nyakati za usiku kutokana na baadhi ya vijana wa kundi hilo kuendesha vitendo vya ukabaji na utumiaji wa madawa ya kulevya.
Thursday, 29 May 2014
'Mbwa mwitu' 10 watiwa mbaroni
01:16
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru