NA RACHEL KYALA
RAIS Jakaya Kikwete, amewaagiza wakuu wa mikoa, madaktari na watendaji, kuhakikisha wanasimamia udhibiti wa vifo vya uzazi na watoto kwa kuwezesha asilimia 80 ya wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya afya.
Ametaka kuwepo na mfumo wa kumpatia taarifa za maendeleo ya mkakati wa kupunguza vifo vya uzazi na watoto katika maeneo yao kila baada ya miezi minne.
Rais Kikwete, alisema hayo jana mjini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa Mpango mkakati wa kuongeza kasi ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga.
Alisema anatambua kuwa wizara ina utaratibu wa kupokea taarifa hizo kila baada ya miezi sita, lakini kutokana na tatizo la vifo hivyo kuwa kubwa na huku muda wa kujipima katika utekelezaji wa malengo ya milenia ukikaribia, ni vyema kuongeza kasi ya kudhibiti.
“Hali bado ni mbaya, taifa letu bado linakabiliwa na kiwango kikubwa cha vifo vya uzazi na watoto wachanga.
“Hili linachangiwa na asilimia 49 ya akina mama kujifungulia kwa wakunga wa jadi,” alisema Rais Kikwete.
Alisema takwimu zinaonyesha ni asilimia 51 tu ya wajawazito ndio wanajifungulia katika vituo vya huduma za afya, ambapo malengo ya milenia yanataka asilimia 80 ifikapo mwakani.
“Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa hadi kuvuka malengo katika mkakati wa kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano, lakini changamoto ipo kwenye vifo vya weajawazito, bado vipo juu kwa wastani 454 kati ya vizazi hai 100,000,” alisema.
Alisema vifo vitokanavyo na uzazi kulingana na malengo ya millennia, vinatakiwa kupungua hadi kufikia 193 kwa kila 100,000.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru